HTM WAPELEKA MAJI KWA WANANCHI,HANDENI NA KOROGWE
Na Yusuph Mussa,DmNewsonline
KOROGWE
MAMLAKA ya Maji na Usafi wa Mazingira HTM - Korogwe wametekeleza jitihada za kufungua huduma ya maji kwenye vijiji vinane (8) na kitongoji kimoja wilayani Handeni, na vitongoji viwili, Mamlaka ya Mji Mdogo Mombo wilayani Korogwe Mkoa wa Tanga.
Vijiji na vitongoji hivyo vilikosa maji kwa vipindi virefu kuanzia mwaka mmoja hadi miaka mitano kwa baadhi ya vijiji. Jitihada za HTM WSSA zimewezesha kupatikana kwa huduma hiyo katika kipindi cha muda mfupi.
Hayo yalisemwa kwenye taarifa iliyotolewa na Menejimenti ya HTM WSSA leo Oktoba 9, 2026 iliyowasilishwa kwa waandishi wa habari.
Taarifa hiyo ilisema nia ya Serikali ni kuona wananchi wote wanapata maji ya kutosha, na hivyo HTM WSAA itaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kufufua huduma kwenye vijiji vyote vilivyokuwa vinahudumiwa na maji na Mradi wa HTM uliojengwa mwaka 1974 na zilizokuwa Mamlaka za Maji za Handeni, Korogwe na Mombo.
Taarifa hiyo pia imeonesha kuwa matarajio ya Menejimenti ni kuhakikisha kuwa maeneo yote yanayohudumiwa na HTM WSSA yanapata huduma ya kuaminika hasa baada ya kukamilika kwa Mradi Mkubwa wa Miji 28 unaotarajiwa kunufaisha wakazi wa Wilaya za Handeni, Korogwe, Muheza na Pangani, pamoja na vijiji vinavyopitiwa karibu na bomba kuu.
Taarifa hiyo ilivitaja vijiji na vitongoji anbavyo kwa muda mrefu vilikosa huduma ya maji, na sasa vinapata maji kuwa ni Magamba kilichopo Kata ya Magamba, Kweditilibe na Kwedibangala, Kata ya Kiva, Nkale, Kata ya Kwamatuku, Komdudu, Kata ya Kwamkono, Mzundu, Kata ya Ndola kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Handeni.
Kwa Halmashauri ya Mji Handeni, maji yamefika Kitongoji cha Mji Mpya, Kata ya Kwamagome, Mtaa wa Msasa, na Kwemgodi, Kata ya Msasa. Kwa upande wa Wilaya ya Korogwe ni vitongoji vya Jitengeni na Mwisho wa Shamba, Mamlaka ya Mji Mdogo Mombo. 






Comments
Post a Comment