UONGOZI WA SHIRIKISHO LA VYAMA VYA TIBA ASILI TANZANIA WADAIWA SI HALALI NA UMEKOSA DIRA YA KUENDESHA VYAMA VYA WAGANGA WA TIBA ASILI
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
UONGOZI wa Shirikisho la Vyama vya Waganga wa Tiba Asili Tanzania (Shivyatiata) uliokasimishwa madaraka ya muda wa mwaka mmoja kuliongoza hadi likae sawa, unalalamikiwa na wachama wa vyama vya waganga wa tiba asili nchini kwa kuhodhi madaraka kwa miaka nane kinyume cha sheria na utaratibu waliokubaliana.
Wakizungumza na Mwandishi wa DMNews online Tanzania Disemba 31, 2025 baadhi ya wanachama wa vyama vya waganga wa tiba asili kutoka vyama 28 vinavyounda shirikisho hilo, kwamba uongozi uliopo si halali wakidai haukuchaguliwa kikatiba.
Pia, wamesema kuwa uongozi huo wa Shirikisho umeshindwa kutimiza majukumu na malengo ya Serikali kuukasimisha madaraka ya muda badala yake unalitumia kujinufaisha wenyewe ikiwamo kufifisha shirikisho kwa kulikosesha dira.
Mwenyekiti wa Umoja wa Watengeneza Bidhaa Asili Tanzania (UWABIATA) Rajab Hamis Ganzi ambaye pia amefukuzwa kwenye shirikisho baada ya kuwa mmoja wa watu walioonyesha msimamo wa kuendeshwa isivyo shirikisho hilo. akizungumzia uhai wa shirikisho amesema kama ni mgonjwa basi shirikisho hilo lipo chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) likisubiri rehema za Mwenyezi Mungu.
“Shivyatiata iliundwa na vyama kati ya 13 au 14, wakati huo mimi nilikuwa chama Cha CHAWAMAMU, kusudio la kuanzishwa kwake liwe msemaji kati ya waganga na serikali pasipo kuvunja vyama vya waganga.
“Baada ya kulisajili Wizara ya mambo ya ndani, uongozi ulipitishwa kwa muda wa mwaka mmoja, tulikutana tukapanga tufanye uteuzi wa kudumu, tukapanga kila chama kichangie Sh milioni moja zipatikane milioni 13 ufanyike uchaguzi.
"Nikiwa Mwenyekiti wa Shivyatiata kwa mkoa wa Dar es Salaam nilifanya jitihada nikakusanya Sh milioni moja, vyama vingine havikuchanga, tukashindwa kufanya uchaguzi na ukawa mwanzo wa kushindwa kuendesha shirikisho,” amesema Hamis.
Pamoja na mambo mengine Hamis amesema viongozi waliokuwa wamepewa jukumu la kuliendesha hawana uelewa wa kutosha wa kuanzishwa kwake kwani tangu awali waliamini kuwa shirikisho ni mali ya serikali na ndio yenye jukumu la kuligharamia.
Hamis amesema ,kitendo cha kuwashauri kuwa wajifunge mkanda ili wafanikishe kusimama kwa shirikisho hilo, amesema ulikuwa mwanzo wa yeye kuchukiwa na uongozi wa Shirikisho ukamfanyia njama za kumfukuza unachama.
Moja ya changamoto anazozitaja kuwa zimesababisha shirikisho hilo kuwepo kama halipo ni pamoja na viongozi hao kutoshaurika, kuendesha mambo bila vikao huku vyama vyote vikiachwa bila dira na mwelekeo sahihi.
Amesema uongozi wa shirikisho ambao hata ofisi zake hazijulikani zilipo umeling’ang’ania shirikisho hilo kwa ajili ya kujinufaisha na fedha zitokanazo na uuzaji vyeti ndio maana hautaki kufanya uchaguzi wala maboresha mahususi ya shirikisho.
Katibu Mkuu Shivyatiata azungumza
Kwaupande wake Katibu Mkuu wa Shivyatiata, Othuman Shem akizungumzia lawama hizo zinazotolewa na wadau wa tiba asili amekiri kuwa walichaguliwa na kupewa madaraka ya muda ya kusimamia na kuandaa mfumo wa kuendesha shirikisho ikiwamo kusimamia uchaguzi wa viongozi nchi nzima.
Amesema kazi hiyo waliifanya lakini mchakato haukukamilika kwa wakati na hata walipoongezewa muda bado lilishindikana kukamilika hali iliyowalazimu kwenda wizara ya mambo ya ndani kueleza hali halisi, ukatolewa waraka uliolekeza namna viongozi watakaoshiriki uchaguzi wa shirikisho.
“Kwa bahati mbaya vyama vyenyewe havikufanya uchaguzi na kuleta viongozi wapya, sasa moja ya tatizo kwanini uchaguzi haufanyiki hadi leo liko hapo, lakini la pili ni kutotimia kwa akidi ya wanachama,” amesema Shem
NKuongeza kuwa ili kufanyika uchaguzi ni lazima akidi ya wanachama wote 275 itimie ambao ni viongozi kutoka Vyama vya Tiba asili Tanzania bara.
Anajivua lawama kwa kueleza kuwa hata Serikali baada ya jambo kulikabidhi kwa Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kuratibu uchaguzi wa viongozi wa vyama vya tiba asili katika ngazi waliyopo nao jukumu hilo liliwashinda kutimiza.
Kutokufanyika kwa uchaguzi wa Shivyatiata.
Amesema kwa kiasi kikubwa pia unakwamishwa na uhaba wa kifedha walio nao viongozi wa vyama akidai kuwa miongoni mwao hutumia fedha zao kuendesha shughuli za shirikisho pamoja na kulalamikiwa kwamba wamehodhi madaraka ya shirikisho ilhali hawana maarifa ya kuliendesha yeye amejitetea kuwa yuko tayari kuondoka madarakani ili watu wengine wasimamie shirikisho hilo nakwamba hata amechoka.
Hata hivyo amesema, “Tunahitaji vijana waingie madarakani, viongozi waliopo kwenye vyama walio wengi ni wazee ambao hawawezi kuendana na kasi ya sasa, nashauri hata vyama vinapochagua viongozi kwa sasa, angalau vijitahidi kuchagua vijana, wazee wabaki kuwa washauri tu,” amesema huku akipendekeza kwenye shirikisho nako iwe hivyo hivyo.
Amekataa hoja ya uongozi kung’ang’ania madaraka kwa sababu ya kupata fedha zitokanazo na vyeti wanavyouza kwa kusema wenyeviti wa vyama wakipewa vyeti hivyo kwenda kuviuza, wakishaviuza fedha hazirudi kwenye shirikisho.
“Isitoshe vyeti vingi vinavyouzwa kwa sasa ni feki, vingi vinavyouzwa ni vilivyogushiwa na kuna baadhi ya watu tumewakamata Tabora, Mwanza na Songea wakivigushi” amesema.
Nakuongeza kuwa shirikisho kwa sasa halitoi vyeti, hivyo tuhuma kwamba uongozi unauza vyeti hazina ukweli wowote na endapo wapo wanaofanya hivyo basi wanatumia mngongo wa shirikisho kujipatia fedha.
Mdau wa tiba asili ambaye pia ni Rais Chama Cha TAMETO, Sharif Wiketye ametoa maoni yake, kuhusu Shivyatiata inavyoendeshwa akidai kuwa uongozi uliopo ni dhaifu na umepita muda wake.Pia, amesema uongozi huo umekiuka hata baadhi ya maazimio yaliyopitishwa na wanachama wa vyama vinavyounda shirikisho kwani tangu limeundwa mawasiliano baina ya viongozi wa shirikisho na vyama hayako vizuri.
“Mwaka 2023 liliitishwa kongamano la waganga wa vyama vya waganga lililoitishwa na baraza la vyama vya tiba asili, moja ya maazimio kwenye kongamano hilo ni kufanyika uchaguzi mkuu wa shirikisho, walipewa miezi sita, lakini tangu hapo mpaka sasa hakuna kauli yoyote imetoka kueleza kwanini uchaguzi haufanyiki na sababu ni ipi,” amesema Wiketye.
Amezipinga sababu zote zinazotolewa na uongozi wa Shirikisho hasa madai ya Katibu Mkuu wa Shivyatiata kuwa shirikisho halina fedha akidai kuwa si za kweli kwa hoja kuwa kama sababu ingekuwa hiyo wangeweza kuitisha mkutano wa vyama vikakutana na kujadili namna ya kupata fedha.
“Sisi Tameto tunaunga mkono sana shirikisho liwepo, sasa katika hali ambayo tunaona mambo hayako sawa, ni lazima tukubali kuwa tunahitaji uchaguzi ufanyike tupate viongoziz wapya, hawa waliopo wakisema wamechoka, wasisubiri ifanyike miujiza ya Mungu, mtu akiona amechoka ajizuru tu,” amesema.
Amesema ni suala la kushangaza kuona hata baada ya Makamu mwenyekiti wa shirikisho kufariki miaka mitatu iliyopita uongozi umeshindwa kuitisha mkutano wala vikao vya kujadili ikiwa Makamu Mwenyekiti ameondoka ni nani awe mbadala hali inayoonyesha kuhitajika mabadiliko ndani ya Shirikisho.

Comments
Post a Comment