MTOTO MCHANGA ACHINJWA,TABORA

 Na Allan Kitwe,DmNewsonline

                 IGUNGA 

MWANAUME mmoja mkazi wa Kijiji cha Imalanguzu, Kata ya Mwamakona, Tarafa ya Igurubi, Wilaya ya Igunga Mkoani Tabora amemchinja mtoto wake mchanga aliyekuwa na umri wa miezi miwili na kumjeruhi vibaya mke wake.

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari leo, Kamanda wa Polisi Mkoani hapa , Richard Abwao ameeleza kuwa tukio hilo limetokea Machi 25 mwaka huu majira ya saa 3 usiku huko katika Kitongoji cha Ibindo, kijiji cha Imalanguzu.

Amebainisha kuwa mwanaume aitwaye Bunzali Jidola (30) Msukuma, mkulima, mkazi wa Imalanguzu alimchinja kwa kutumia kitu chenye ncha kali mtoto wake aitwaye Dorcas Bunzali aliyekuwa na umri wa miezi miwili.

Ameongeza kuwa baada ya mauaji hayo alimjeruhi pia mke wake aitwaye Jeni Ndaki (24) Msukuma, mkulima, mkazi wa Kijiji cha Ibutamisuzi kwa kutumia kifaa hicho chenye ncha kali na kisha kutokomea kusiko julikana.

Amesema majeruhi huyo aliokolewa na wasamaria wema na kukimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Nkinga iliyoko Wilayani humo baada ya kupatiwa karatasi ya PF3 na Polisi, hadi sasa anaendelea na matibabu ila hali yake sio nzuri.

Kamanda ameeleza kuwa baada ya sungusungu waliokuwa zamu usiku huo kufanya ufuatiliaji walifanikiwa kumkuta mtuhumiwa akiwa amejinyonga kwa kutumia shuka kwenye nguzo ya umeme wa Tanesco katika kijiji hicho cha Imalanguzu.  

Amefafanua chanzo cha tukio hilo la kusikitisha kuwa ni wivu wa kimapenzi, kwani mtuhumiwa alifanya mauaji hayo baada ya kutokuwepo maelewano na mke wake huku akihisi kuwa mtoto huyo sio wake.

Na kubainisha kuwa marehemu ametekeleza tukio hilo ikiwa ni siku mbili tu baada ya kurejea kutoka kwenye shughuli zake za machimbo ya dhahabu eneo la  Bulangamilwa namba 6, katika Kata ya Choma Wilayani humo .

Amedokeza kuwa marehemu alikwenda kwenye shughuli zake hizo tangu mwezi wa Nane mwaka jana na aliporudi akakuta mke wake ana mtoto mchanga, hivyo akahisi kuwa alipewa mimba na mwanaume mwingine.

Comments

Popular posts from this blog

UONGOZI WA SHIRIKISHO LA VYAMA VYA TIBA ASILI TANZANIA WADAIWA SI HALALI NA UMEKOSA DIRA YA KUENDESHA VYAMA VYA WAGANGA WA TIBA ASILI

DKT. KIJAZI KUSIMAMIA MIRADI YA MAENDELEO JIMBO LA KOROGWE MJINI.