KILA KUNDI LINAHITAJI AMANI,VIONGOZI WA DINI IOMBEENI NCHI.
Na Yusuph Mussa,DmNewsonline
Handeni
WAZIRI Mkuu wa Tanzania Dkt. Mwigulu Nchemba amewaomba viongozi wa dini kuendelea kuiombea amani ya nchi iendelee kuwepo, kwani kila kundi kwenye jamii ili kuweza kutekeleza majukumu yake, linahitaji amani.
Ameyasema hayo Oktoba 4, 2026 kwenye Ibada ya kumuweka Wakfu na kumuingiza kazini Askofu wa Dayosisi mpya ya Handeni ya Kanisa la Anglikana Tanzania Charles Mika Lundu, iliyofanyika Kanisa Kuu la Kristo Mfalme, Chanika wilayani Handeni mkoani Tanga.
Dkt. Mwigulu alisema sio wakulima, wafanyabiashara wala wavuvi wanaohitaji uwepo wa amani, bali wananchi wote wakiwemo wanasiasa na viongozi wa dini, wote wanaitegemea amani ili kuweza kuendesha mambo yao.
Alisema wapo watu kutoka mataifa mengine, wangependa kuzaliwa Tanzania ili kunufaika na amani hiyo, hivyo Watanzania wajione ni watu wenye bahati kwa kuendelea kuitunza amani.
"Tuiombee nchi yetu, na tumuombee Rais wetu (Dkt. Samia Suluhu Hassan). Tumepewa na Mungu nchi nzuri yenye historia nzuri ambayo mataifa mengi wangetamani kuwa Watanzania, hivyo viongozi wa dini muendelee kutuombea. Sisi upande wa Serikali tutaendelea kutimiza wajibu wetu kuona amani, mshikamano na utulivu vinaendelea kuwepo.
Dkt. Mwigulu amewataka wazazi kuwa walezi wa watoto wao wote wa kike na kiume, kwani wakati wao wanakuwa, kwenye jamii watoto wa kike ndiyo walionekana wapo kwenye hatari zaidi, lakini kwa sasa hata watoto wa kiume wapo kwenye hatari. Hivyo jamii imetakiwa kushirikiana ili kuona watoto na vijana, wote wanakuwa salama.
Dkt. Mwigulu aliwakumbusha wananchi juu ya tishio la El- Nino, kwani pamoja na kwamba tunamtegemea Mungu kwenye mambo yote, na akiamua kutulinda anaweza, lakini tusiwapuuze Wanasayansi, hivyo watu waliopo maeneo hatarishi waondoke ama kuchukua tahadhari za kutosha.
Waziri Mkuu alimpongeza Askofu mpya na Dayosisi mpya ya Handeni, Lundu, akisema amepewa dhima kubwa ya kuwaongoza waumini wa kanisa hilo kwenye wilaya za Handeni, Pangani na sehemu ya maeneo ya Wilaya ya Kilindi, huku akisema kanisa lina historia ya zaidi ya miaka 100 nchini.
Dkt. Mwigulu katika kuunga mkono ujenzi wa Kitega Uchumi cha Kanisa Anglikana, ameahidi kutoa sh. milioni 50 kwa ajili ya ujenzi huo, kwani kwa sasa sio Serikali tu, hata taasisi za dini zinatakiwa kujitegemea kiuchumi. Ni baada ya wafadhili kukata misaada maeneo mengi.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya hafla hiyo, Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania Dkt. Maimbo Mndolwa aliwataka Watanzania kulinda amani, huku akiwataka Watanzania kulinda amani ya nchi.
Askofu Dkt. Maimbo, pia aliwataka waumini kuomba ili Mungu aweze kuepusha mvua nyingi zinazotarajiwa kunyesha kuanzia katikati ya Oktoba, mwaka huu hadi Januari mwakani. 























Comments
Post a Comment