WAKULIMA KOROGWE WATOA USHUHUDA WALIVYONUFAIKA NA FORLIVES


  Wakulima wa Kikundi cha Vugiri Farmers Group wakiwa kazini.


 Na Yusuph Mussa,DmNewsonline

            KOROGWE 

BAADHI ya wakulima wa mahindi., maharage, viungo na mbogamboga wa Kijiji cha Vugiri, Kata ya Vugiri, Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga wameelezea mafanikio yao baada ya kuwezeshwa na Mradi wa FORLIVES.

Wakulima hao walitoa ushuhuda wao Septemba 4, 2026 mbele ya vijana sita kutoka vyuo na maeneo mbalimbali nchini Denmark kupitia kikundi chao cha Global Story Tellers, wanaotembelea miradi yote Tanzania inayofadhiliwa na Shirika la kidini la Danmission, na kwa Wilaya ya Korogwe, taasisi hiyo kupitia Shirika la Uhifadhi wa Misitu ya Asili Tanzania (TFCG), inafadhili Mradi wa Tunza Uumbaji (Care for Creation).

Mkulima wa Vugiri Lishe Group, Judithi Ngomo, alisema Mradi wa FORLIVES  uliwawezesha wananchi kiuchumi kwa kuwapa elimu ya kilimo cha mbogamboga, maharage, mahindi, viungo, ufugaji wa nyuki, kuwapa vifaa kwa ajili ya ulinzi wa misitu na mazingira yake. Nia ni wawe na shughuli mbadala, badala ya kutegemea rasilimali za misitu kama mbao na kuni ili kuendesha maisha yao.

"Pamoja na kuwa na kikundi chetu cha Vugiri Lishe Group, pia nina shamba langu la mbogamboga ambalo linaniwezesha kupata mboga za kuuza na kutumia nyumbani. Na matarajio yangu ni kuona kwa kupitia kilimo hiki nasomesha watoto wangu wote, na pia kuweza kujenga nyumba yangu nzuri" amesema Ngomo

Mkulima Henry Shelugendo wa Vugiri Farmers Group alisema wamepata mafanikio kwa kuwepo Mradi wa FORLIVES ambao uliwasaidia kuweza kuanzisha mashamba na bustani kwa ajili ya mazao mbalimbali, na wamefanikiwa kuboresha maisha yao kwa miradi ya kilimo, na kwa ujio wa Mradi wa Tunza Uumbaji utawaongezea mafanikio kwenye kilimo.

"Kabla ya hapo tulikuwa tunalima bila ufanisi sababu tulikuwa hatutumii matuta. Lakini baada ya kuja kwa Mradi wa FORLIVES, umetuwezesha vitu vingi ikiwemo kilimo cha kutumia makinga maji (matuta), na hiyo ni kutokana na ardhi yetu kuwa na miinuko. Hivyo tunaamini, kwa kuja Mradi wa Tunza Uumbaji utatuongezea maarifa zaidi kwenye kilimo" alisema Shelugendo.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Vugiri Julius Mntambo alisema waliupokea Mradi wa FORLIVES ambao ndani yake wananchi walibuni miradi mingi ikiwemo ya kilimo cha mbogamboga, maharage, viungo, ufugaji wa nyuki, upandaji wa miti, na uhifadhi wa misitu ya asili, na miradi yote imefanikiwa.

"Wananchi wangu walinufaika sana na miradi iliyoanzishwa na kuwezeshwa na FORLIVES. Na kwa sasa tuna Mradi wa Tunza Uumbaji. Mradi huu kwetu ni muendelezo wa mradi wa kwanza wa FORLIVES, hivyo tunaahidi kuendeleza kile tulichokianzisha miaka mitatu iliyopita. Tukiwa tunawaaga, tunaomba muendelee kutukumbuka kwa kuweza kuja siku nyingine" amesema Mntambo.

Akizungumza kwenye ziara hiyo mbele ya wakulima, Meneja wa TFCG Wilaya ya Korogwe Bettie Luwuge alisema vijana hao wanatembelea miradi mbalimbali inayofadhiliwa na Danmission kwenye Wilaya ya Korogwe ikiwemo ya kilimo, misitu ya uhifadhi na mizinga ya nyuki.

"Nchi ya Denmark wana utaratibu vijana wao wakiwa vyuo ama wakimaliza, wanawaachia kwenda duniani kujifunza mambo mbalimbali, na kuona dunia inafanyaje, lakini kwenye maeneo ambayo wanatoa fedha zao. Sisi Korogwe, sisi Vugiri ni sehemu ya wanufaika. Kwa hiyo wanawaachia vijana ili waangalie ni vipi fedha zao zinavyotumika,  wananchi wanafurahi vipi, wanufaika wanasemaje namna tunavyoendelea nao" amesema Luwuge.

Luwuge ambaye pia ni Mratibu wa Mradi wa Tunza Uumbaji, alisema vijana hao pamoja na kuangalia miradi inayofadhiliwa na Danmission, pia wanajifunza tamaduni, mila na desturi za wenyeji. Lakini pia wanaangalia mazingira na fursa zinazowazunguka wenyeji wa maeneo husika, hivyo wakifika kwao wanawatangazia kwenye majukwaa mbalimbali ikiwemo makanisani kwa yale waliyoyaona, hivyo kuweza kuleta fedha nyingine.

Vijana hao, pamoja na kutembelea mashamba ya wakulima wa vijiji vya  Vugiri na Bagamoyo, pia walitembelea na kuona ufugaji wa nyuki kwa ajili ya asali, lakini pia walitembelea na kuona uhifadhi wa misitu ya asili kwenye vijiji hivyo. Pia walipanda Mlima Shemkilimo wenye urefu wa mita 3,000 uliopo Kijiji cha Vugiri, na kujionea mandhari wakiwa kileleni, huku wakiuona Mji wa Korogwe na viunga vyake.
Wakulima wa Kikundi cha Vugiri Lishe Group wakipanda miche ya mbogamboga wakiwa na vijana kutoka Denmark.   
Mkulima Henry Shelugendo wa Vugiri Farmers Group akifanyiwa mahojiano.

Mkulima wa Vugiri Lishe Group, Judithi Ngomo akifanyiwa mahojiano.


Comments

Popular posts from this blog

MWAKIPOSA ASHINDA NAFASI YA UWENYEKITI WA WENYEVITI WA SERIKALI YA MTAA MKOA WA DAR ES SALAAM

UONGOZI WA SHIRIKISHO LA VYAMA VYA TIBA ASILI TANZANIA WADAIWA SI HALALI NA UMEKOSA DIRA YA KUENDESHA VYAMA VYA WAGANGA WA TIBA ASILI

WAMILIKI WAMASHAMBA SOMELO_ ZINGIZIWA WAJA JUU WASEMA KUNA MTU ANATAKA KUPORA MAENEO YAO ,WATISHIA KWENDA MAHAKAMI.