VIJANA WA DENMARK WASHIRIKI MSALAGAMBO KOROGWE
Meneja wa TFCG Wilaya ya Korogwe Bettie Luwuge (katikati) akizungumza na wakulima wa Vugiri.
Na Yusuph Mussa, DmNewsonline
KOROGWE
VIJANA sita kutoka nchini Denmark
wameshiriki kilimo cha msalagambo (pamoja) na wakulima wa mahindi., maharage na mbogamboga wa Kijiji cha Vugiri, Kata ya Vugiri, Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga.
Pamoja na mambo mengine, vijana hao kutoka vyuo na maeneo mbalimbali nchini Denmark kupitia kikundi chao cha Global Story Tellers, wanatembelea miradi yote Tanzania inayofadhiliwa na Shirika la kidini la Danmission, na kwa Wilaya ya Korogwe, taasisi hiyo kupitia Shirika la Uhifadhi wa Misitu ya Asili Tanzania (TFCG), inafadhili Mradi wa Tunza Uumbaji (Care for Creation).
Mradi huo kwa Wilaya ya Korogwe, unajishughulisha na uhifadhi wa misitu ya asili na mazingira.kwa kuwawezesha wananchi kiuchumi kwa kuwapa elimu ya kilimo cha mbogamboga, maharage, mahindi, ufugaji wa nyuki, kuwapa vifaa kwa ajili ya ulinzi wa misitu na mazingira yake. Nia ni wawe na shughuli mbadala, badala ya kutegemea rasilimali za misitu kama mbao na kuni ili kuendesha maisha yao.
Akizungumza Septemba 2, 2026 kwenye ziara hiyo mbele ya wakulima, Meneja wa TFCG Wilaya ya Korogwe Bettie Luwuge alisema vijana hao watatembelea miradi mbalimbali inayofadhiliwa na Danmission Wilaya ya Korogwe ikiwemo ya kilimo, misitu ya uhifadhi na mizinga ya nyuki.
"Nchi ya Danmark wana utaratibu vijana wao wakiwa vyuo ama wakimaliza, wanawaachia kwenda duniani kujifunza mambo mbalimbali, na kuona dunia inafanyaje, lakini kwenye maeneo ambayo wanatoa fedha zao. Sisi Korogwe, sisi Vugiri ni sehemu ya wanufaika. Kwa hiyo wanawaachia vijana ili waangalie ni vipi fedha zao zinavyotumika, wananchi wanafurahi vipi, wanufaika wanasemaje namna tunavyoendelea nao" amesema Luwuge.
Luwuge ambaye pia ni Mratibu wa Mradi wa Tunza Uumbaji, alisema vijana hao pamoja na kuangalia miradi inayofadhiliwa na Danmission, pia wanajifunza tamaduni, mila na desturi. Lakini pia wanaangalia mazingira na fursa zinazowazunguka wenyeji wa maeneo husika, hivyo wakifika kwao wanawatangazia kwenye majukwaa mbalimbali ikiwemo makanisani kwa yale waliyoyaona, hivyo kuweza kuleta fedha nyingine.
Mkulima Henry Shelugendo wa Vugiri Farmers Group alisema wamepata mafanikio kwa kuwepo Mradi wa FORLIVES ambao pia ulifadhiliwa na Danmission, uliwasaidia kuweza kuanzisha mashamba na bustani kwa ajili ya mazao mbalimbali, na wamefanikiwa kuboresha maisha yao kwa miradi ya kilimo, na kwa ujio wa Mradi wa Tunza Uumbaji utawaongezea mafanikio kwenye kilimo. 










Comments
Post a Comment