KILINDI BARABARA BADO NI CHANGAMOTO

 Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi, Dkt. Michael Chabai.

 Na Yusuph Mussa,DmNewsonline

                KILINDI

MWENYEKITI wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi mkoani Tanga, Dkt. Michael Chabai amesema barabara za wilaya hiyo bado ni changamoto, na kueleza moja ya sababu ya wakulima kuuza mazao yao kwa bei ya chini ni kutokana na changamoto ya barabara hizo.

Ameyasema hayo Agosti 22, 2026 wakati anafungua kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo, na kuongeza kuwa jitihada zinahitajika kwa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kuhakikisha wanafanyia matengenezo ya mara kwa mara barabara za vijijini ili kuona wakulima wanakuwa na uwezo wa kwenda kuuza  mazao yao sokoni.

"Barabara zetu kwenye wilaya yetu bado ni changamoto, na hii inasababisha mazao ya wakukima wetu kuuzwa kwa bei ya chini. Hivyo tunataka kuona barabara hizo zinapitika ili wakulima wetu waweze kufikisha mazao yao sokoni" alisema Dkt. Chabai.

Dkt. Chabai ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Negero, amesema pamoja na changamoto hiyo ya barabara, wakulima wasikubali kuuza mazao yao kwa bei ya chini, ama kuuza kwa ajili ya anasa, bali wakiamua kuuza, wauze kwa ajili ya mahitaji muhimu kwa ajili ya familia zao. Ni baada ya Wilaya ya Kilindi kuonesha mwaka huu wamepata mazao mengi hasa mahindi na maharage.

"Miaka inayotanguliwa na mavuno makubwa, ndiyo miaka inayofuatiwa na njaa kubwa. Na mara nyingi anaeuza anasema chakula kimepatikana kwa wingi, hivyo anaendelea kuuza. Tumepata chakula kingi sana, lakini wananchi wauze kwa faida, wauze kwa ajili ya kupata mahitaji muhinu, lakini pia wauze kwa tahadhari kwa ajili ya kuweka akiba ya chakula" amesema Dkt. Chabai.

Dkt. Chabai alisema suala la ukusanyaji mapato kwenye halmashauri hiyo linatakiwa lipewe kipaumbele ili kuona halmashauri hiyo inaendelea kukusanya mapato yatakayowezesha kukamilisha miradi iliyoanzishwa na wananchi, lakini pia miradi mipya.

Kwenye maswali ya papo kwa hapo, Diwani wa Viti Maalumu, Hamida Kidunda alisema pamoja na jitihada za Serikali kuendelea kuongeza walimu, lakini wilaya hiyo bado inakabiliwa na uhaba wa walimu hasa shule za msingi, hivyo kutaka kujua ni lini halmashauri hiyo itafanya msawazo wa walimu.

"Swali la nyongeza; kutokana na umuhimu wa walimu wanawake shuleni kwa watoto wote, na zaidi mtoto wa kike, je ni lini halmashauri itafanya msawazo wa walimu wanawake. Hii ni kutokana na baadhi ya shule kukosa kabisa walimu wa kike, na wote tunajua walimu wa kike pia ni walezi wetu kwa watoto wa kike wakiwa shuleni" amesema Kidunda.

Naye Diwani wa Kata ya Mkindi, Hilary Msigwa aliuliza ni lini halmashauri itatekeleza Mradi wa Bwawa la Mifugo Kijiji cha Lengusero, huku Diwani wa Kata ya Kibirashi akitaka kujua halmashauri ina mpango gani katika kujenga Kituo cha Afya Kibirashi, kwani ni kero kubwa kwa wananchi wa kata hiyo wanaozidi 30,000.

Akijibu hoja za madiwani, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Nhojo Kushoka alisema hadi sasa halmashauri hiyo ina shule za msingi143 ikiwa shule 136 za Serikali,na saba za binafsi, na zina wanafunzi jumla ya 79,919. Mahitaji ya walimu ni 2,044 wakati waliopo ni 972, upungufu ikiwa ni 1,028.

"Hivyo kutokana na upungufu wa kila shule wa walimu inakuwa ni vigumu kuhamisha, lakini kupitia ajira mpya, tutaendelea kurekebisha ikama ili kukidhi mahitaji ya kila shule. Mpaka sasa walimu wanadai halmashauri fedha za uhamisho sh. 268,307,000, na pindi fedha ikiletwa, ikama itarekebishwa" amesema Kushoka.

Kushoka alisema Mradi wa Bwawa la Mifugo Lengusero unatekelezwa chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi. Na mpaka sasa Usanifu umekwishafanyika. Hivyo, halmashauri inaendelea kufuatilia na kukumbusha ili utekelezaji wa mradi huo uweze kuanza.

Kushoka alisema kuhusu Kituo cha Afya Kibirashi, halmashauri inaandaa Andiko kwa ajili ya kuomba fedha TAMISEMI kwa ajili ya kituo cha afya. Aidha, kwa mwaka wa fedha 2027/2028 wanatenga fedha kutoka mapato ya ndani kwa ajili ya ujenzi huo.

Wakati huo huo, Meneja wa Benki ya CRDB Tawi la Kilindi, Ronald Paul amewaeleza madiwani kuwa wanaweza kukopa fedha kwenye benki hiyo wakiwa kama madiwani, wakulima ama wajasiriamali, huku akiwataka kwenda kuwaeleza wananchi wao kuwa benki hiyo ina fursa nyingi.

Paul alisema benki hiyo inatoa mikopo pia kwa shughuli za kilimo kuanzia kulima, kupanda hadi kuvuna. Lakini pia inakopesha vitendea kazi kuanzia bodaboda, guta na trekta, hivyo kumrahisishia mkulima kuweza kulima kisasa na kufikisha mazao yake sokoni.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi, Nhojo Kushoka.   
Diwani wa Kata ya Mkindi, Hilary Msigwa.

        
Meneja mpya wa Benki ya CRDB, Tawi la Kilindi, Ronald Paul.
Diwani wa Viti Maalumu, Hamida Kidunda.

Comments

Popular posts from this blog

UONGOZI WA SHIRIKISHO LA VYAMA VYA TIBA ASILI TANZANIA WADAIWA SI HALALI NA UMEKOSA DIRA YA KUENDESHA VYAMA VYA WAGANGA WA TIBA ASILI

MWAKIPOSA ASHINDA NAFASI YA UWENYEKITI WA WENYEVITI WA SERIKALI YA MTAA MKOA WA DAR ES SALAAM