ZANZIBAR YAPEWA FURSA YA KUWA MWENYEJI WA TUZO ZA 33 ZA WORLD TRAVEL AWARDS
Na Mwandishi wetu,DmNewsOnline
DAR ES SAAM
ZANZIBARA imepewa fursa ya kuwa mwenyeji wa Tuzo za 33 za World Travel Awards, hatua inayolenga kuongeza utambulisho wa visiwa hivyo katika ramani ya utalii duniani na kufungua zaidi fursa za uwekezaji katika sekta hiyo.
Zanzibar inatarajia kupokea zaidi ya wageni 250 kutoka mataifa mbalimbali watakaoshiriki katika hafla hiyo, wakiwemo wawekezaji katika sekta ya hoteli pamoja na wawakilishi wa mashirika ya ndege.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Agosti 24, 2026, Mwenyekiti wa Bodi ya Kamisheni ya Utalii Zanzibar, Suleiman Ali Mohamed, amesema kuwa kuwa mwenyeji wa tuzo hizo ni fursa kubwa kwa Zanzibar kutangaza vivutio vyake vya utalii, kukuza uwekezaji na kuhakikisha wananchi wananufaika na sekta hiyo kupitia dhana ya utalii endelevu.
Amesema Serikali inaendelea kuimarisha miundombinu ya utalii ili kuwezesha sekta hiyo kukua zaidi na kuongeza mchango wake katika uchumi wa Zanzibar, huku akieleza kuwa tukio hilo linatarajiwa kutoa fursa kwa wadau mbalimbali kuona uwezo na fursa zilizopo katika sekta ya utalii.
Katika mashindano hayo, Zanzibar inashiriki kupitia hoteli 17 pamoja na maeneo matatu ya utalii, huku ikiwakilishwa katika vipengele kati ya 20 na 21 vya tuzo hizo.
Suleiman amewashukuru wananchi kwa kushiriki kupiga kura katika mashindano hayo yaliyofunguliwa Machi mwaka huu na kufungwa Julai 17, akieleza matumaini kuwa Zanzibar itaibuka na tuzo katika baadhi ya vipengele ilivyoshiriki.
Amesema ushindi katika tuzo hizo utaongeza zaidi utambulisho wa Zanzibar kimataifa, sambamba na kusaidia kuvutia watalii na wawekezaji wapya katika sekta ya utalii.
Tuzo hizo zitafanyika nchini Tanzania, huku Zanzibar ikiwa mwenyeji wa World Travel Awards Africa Gala Ceremony 2026, hafla inayotarajiwa kufanyika Agosti 28, 2026 katika Hoteli ya Diamonds Bijoux Zanzibar.

Comments
Post a Comment