URAMBO WAFURAHIA MRADI WA KUPUNGUZA VIFO VYA WATOTO
Na Allan KitweDmNewsonline
URAMBO
WANANCHI Wilayani Urambo Mkoani Tabora wameeleza kufurahishwa na uamuzi wa Serikali ya Awamu ya Sita kupeleka zaidi ya shilingi mil 660 kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa kupunguza vifo vya watoto wachanga.
Akizungumza mbele ya Wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Mkoa waliokuwa katika ziara ya siku moja Wilayani humo jana Mbunge wa Jimbo hilo Magreth Sita ameeleza kuwa mradi huo utasaidia sana kupunguza vifo vya watoto wachanga.
‘Tunamshukuru sana Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutuletea kiasi hicho ili kujengwa mradi utakaohudumia watoto wa changa (NICU) katika Wilaya yetu’, ameeleza.
Amefafanua manufaa mengine ya mradi huo kuwa ni kusogeza huduma za afya ya mtoto karibu zaidi na wananchi na kupunguza rufaa za kwenda Hosptali ya Mkoa.
Faida nyingine ni kuboreshwa huduma za afya kwa watoto wachanga wakiwemo waliozaliwa njiti, wenye ulemavu, wenye matatizo ya kupumua na ya kimaumbile na kuboresha miundombinu ya hospitali hiyo.
Mfanyabiashara Mussa Mohamed ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya hiyo amemshukuru Rais Samia na kubainisha kuwa mradi huo ni mkombozi kwa wana Urambo.
Akiongea kwa niaba ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa, Said Juma Nkumba, Mjumbe wa Kamati hiyo, Janath Kayanda ameguswa sana na mradi huo na kubainisha kuwa utasaidia kuokoa maisha ya watoto.
Ameshauri miradi yote inayojengwa katika maeneo ya wazi kuzungushiwa uzio ili kulinda mipaka yake na kuepusha migogoro itokanayo na uvamizi wa ardhi ili wananchi waendelee kunufaika.
Wakiwa Wilayani humo Wajumbe wa Kamati ya Siasa pia wametembelea mradi wa ujenzi wa Kituo cha Kukusanya na Kuchakata Asali kinajengwa na serikali kwa kushirikiana na wadau kwa gharama ya zaidi ya shilingi milioni 200.
Naye Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (MNEC) Mohamed Nassoro Hamdan ameeleza kuwa mradi huo ni muhimu sana kwa kuwa utaongeza thamani ya zao hilo hivyo kuinua wananchi.
Aidha ameongeza kuwa mradi huo utaleta tija kubwa kwa uchumi wa wananchi na kuchangia pato la taifa, hivyo akashauri utekelezaji wake ukamilike haraka ili wananchi wanaofanya shughuli ya utundikaji mizinga waanze kunufaika. 





Comments
Post a Comment