SHULE YA ELIMU MAALUMU SIKONGE YABORESHWA
Na Allan Kitwe, DmNewsonline
TABORA
SERIKALI imepeleka zaidi ya shilingi milioni 100 Wilayani Sikonge Mkoani Tabora ili kuifanyia maboresho makubwa miundombinu ya shule ya msingi Sikonge inayotoa elimu maalumu kwa watoto wenye ulemavu.
Miundombinu ya shule hiyo yenye watoto 144 (wavulana 92 na wasichana 52), iliyoanzishwa mwaka 2011 Wilayani humo ilikuwa imechakaa sana hali iliyopelekea mazingira yake kutokuwa rafiki kwa watoto wenye mahitaji maalumu.
Akitoa taarifa ya shule kwa Wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Mkoa kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Seleman Pandawe, Katibu wa Kamati ya Ujenzi Makanika Kajuni ameishukuru serikali kwa kuwapatia fedha hizo.
Ameeleza kuwa walipokea kiasi cha shilingi mil 112.2 mwezi Julai 2025 ambazo zimewezesha kujengwa vyumba 4 vya madarasa ya kisasa, kukarabati miundombinu iliyochakaa ikiwemo uzio na geti, kwa sasa shule inang’aa.
Mbunge wa Jimbo la Sikonge, Mhandisi Amos Maganga amesema kuwa wana kila sababu ya kuishukuru serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha mandhari ya shule hiyo, sasa imekuwa ya kimataifa.
‘Ukarabati wa shule hii umekuwa mkombozi kwa watoto wenye mahitaji maalumu kwa kuwa wanapata elimu bora katika mazingira bora ya kujifunzia na ufundishaji, na baadhi yao wameenda hadi chuo kikuu’, ameongeza.
Akitoa salamu za Chama kwa niaba ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa, Komredi Said Nkumba na Wajumbe wote wa Kamati hiyo, Mwenyekiti wa UWT Mkoa Mwanne Mchemba ameeleza kuridhishwa na maboresho makubwa yaliyofanyika.
‘Maboresho haya ni utekelezaji ilani ya uchaguzi ya Chama, tunamshukuru sana Mwenyekiti wa CCM Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kusimamia ipasavyo utekelezaji ilani’, ameongeza.
Amefafanua kuwa kujengwa kwa shule hiyo ni kielelezo cha dhamira njema na ya dhati ya serikali kuhakikisha watoto wote wakiwemo wenye mahitaji maalumu wanapata haki ya msingi ya elimu katika mazingira bora na salama.
Ametoa wito kwa wazazi, walezi na jamii kwa ujumla mahali popote hapa nchini kuleta watoto wao wenye mahitaji maalumu katika shule hiyo ili wapate elimu bora itakayowasaidia kutimiza ndoto za maisha yao. 





Comments
Post a Comment