MEYA KIBAHA AHIMIZA UKAMILISHAJI WA UJENZI WA ZAHANATI YA VISIGA ILI IPANDISHWE HADHI KUWA KITUO CHA AFYA
KIBAHA
MSTAHIKI Meya wa Manispaa ya Kibaha, Dkt. Mawazo, amemtaka Mganga Mkuu wa Manispaa Dkt. Catherine Saguti kuhakikisha ujenzi wa majengo mbalimbali katika Zahanati ya Visiga unakamilika kwa haraka ili zahanati hiyo ipandishwe hadhi na kuwa Kituo cha Afya, hatua itakayowasogezea wananchi huduma bora za afya karibu na makazi yao.
Dkt. Mawazo ametoa wito huo jana alipokuwa katika ziara ya Kamati za Kudumu za Baraza la Madiwani wa Manispaa ya Kibaha zilizotembelea miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo tofauti ya manispaa hiyo.
Amesema ni muhimu kukamilisha kwa wakati mradi wa ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje (OPD) pamoja na miundombinu mingine ya msingi ili kukidhi vigezo vya kuipandisha hadhi Zahanati ya Visiga kuwa Kituo cha Afya.
"Ujenzi huu ukikamilika utarahisisha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi wa Visiga na maeneo ya jirani, hivyo kupunguza adha ya kusafiri umbali mrefu kufuata huduma," amesema Dkt. Mawazo.
Meya amempongeza Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha Dkt. Rogers Shemwelekwa kwa mikakati madhubuti ya kutumia mapato ya ndani kuboresha sekta ya afya kupitia ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya kutolea huduma.
Amesema mafanikio hayo tayari yameonekana kupitia ujenzi wa Kituo cha Afya Kongowe, ujenzi wa Zahanati ya Kilimahewa, pamoja na upanuzi unaoendelea katika Zahanati ya Visiga, miradi inayotekelezwa kwa fedha za mapato ya ndani ya Manispaa ya Kibaha.
Wananchi wanatarajia kuwa kukamilika kwa miradi hiyo kutaimarisha upatikanaji wa huduma za afya na kuongeza ubora wa huduma zinazotolewa kwa wakazi wa Manispaa ya Kibaha. 






Comments
Post a Comment