DC NZEGA ATOA OFA YA ELIMU KWA WATOTO WASIO NA UWEZO
Na Allan Kitwe,DmNewsonline
TABORA
WILAYA ya Nzega Mkoani Tabora imetangaza ofa ya elimu kwa watoto wote wanaochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza na wale wanaochaguliwa kuingia kidato cha tano watakaoshindwa kuripoti shuleni kwa kukosa mahitaji muhimu.
Ofa hiyo imetangazwa na Mkuu wa Wilaya hiyo Naitapwak Tukai alipokuwa akiongea na wananchi kwenye ziara ya Kamati ya Siasa iliyotembelea na kukagua mradi wa shule mpya ya Sekondari ya Kampala iliyopo katika Kata ya Ndala.
Amesema kuwa shule hiyo iliyogharimu zaidi ya shilingi milioni 300 imekamilika kwa asilimia 100 na imejengwa kwa ubora wa hali ya juu, hali itakayosaidia watoto kusomea kwenye shule yenye mazingira bora zaidi.
Mkuu huyo wa Wilaya amesisitiza kuwa wamejipanga vizuri ili kuhakikisha watoto wote wanaochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza na wale wanaochaguliwa kuendelea kidato cha tano wanaripoti katika shule zao pasipo kukosa.
‘Mtoto yeyote atakayeshindwa kuripoti kwa kukosa mahitaji muhimu ya shule tutampatia mahitaji yote ili asikosea fursa hii ya kielimu, katika hili tumejipanga vizuri, hakuna mtoto atakayeachwa nyuma bila elimu, tutamsaidia,’ amesema.
Amewashukuru wadau wa elimu Wilayani humo ambao wamekuwa wakiguswa na hili na kumuunga mkono kwa kutoa michango mbalimbali ili kusaidia watoto wote wanaoshindwa kuendelea na masomo kwa kukosa mtu wa kuwasaidia.
‘Katika hili, naomba Wabunge wetu, Wakurugenzi wa Halmashauri, Wataalamu na Viongozi wote tushikamane na kuwachangia watoto wetu ili kuhakikisha wanapata elimu stahiki ili waweze kutimiza ndoto za maisha yao’, amebainisha.
Amepongeza serikali ya awamu ya sita kwa kutoa fedha za kutosha kwa ajili kuifanyia maboresho makubwa miundombinu ya shule zote ikiwemo kujengwa shule mpya katika maeneo yenye msongamano mkubwa wa watoto.
Mbunge wa Jimbo la Nzega Vijijini Netto Kapalata ameeleza kufurahishwa na uamuzi wa serikali wa kuwapatia shilingi mil 342 .9 kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo mpya na ya kisasa ili kusaidia watoto wasitembee umbali mrefu.
Ameahidi kuunga mkono juhudi za Mkuu wa Wilaya kwa kuhakikisha watoto wote wasio na uwezo wa kumudu mahitaji ya shule wanawezeshwa kupata elimu, alitoa wito kwa wazazi na walezi kutozuia watoto wao kwenda shule. 






Comments
Post a Comment