18 WANASWA NA POLISI KWA MAKOSA YA UHALIFU
Na Allan Kitwe DmNewsonline
TABORA
JESHI la Polisi Mkoani Tabora limefanikiwa kunasa watuhumiwa 18 waliokuwa wakijihusisha na vitendo mbalimbali vya kihalifu ikiwemo mauaji na kuwafikisha mahakamani, miongoni mwao sita wamehukumiwa kunyongwa hadi kufa.
Hayo yamebainishwa leo na Kamanda wa Polisi Mkoani hapa ACP Twaha Lulengelule alipokuwa akiongea na waandishi wa habari katika ukumbi wa Polisi wa Elangwa Shahidi kwenye hafla maalumu ya kujitambulisha kwa wanahabari.
Amefafanua kuwa watuhumiwa hao wamekamatwa katika kipindi cha mwezi Juni na Julai 2026 kutokana na oparesheni, doria na misako mbalimbali iliyofanywa na Jeshi hilo katika Wilaya zote za Mkoa huo ili kukabiliana na vitendo vya uhalifu.
Katika msako wa Juni 18, 2026 majira ya saa 8:00 mchana huko Wilayani Sikonge walikamatwa watuhumiwa 4 wakiwa na silaha 1 aina ya Rifle Model 70-458 isiyo na namba ikiwa na risasi 3, wakiwa katika Pori la Nkomango, tarafa ya Kiwele.
Wengine 9 walikamatwa katika maeneo mbalimbali ya Mkoa huo wakiwa na jumla ya kilo 117 na kete 2062 za dawa za kulevya aina ya bangi, wote wako mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.
Kamanda Lulengelule ameeleza kuwa katika oparesheni iliyofanyika kati ya Juni 17 na Julai 19, 2026 jumla ya watuhumiwa 6 walikamatwa kwa makosa ya mauaji na kufikishwa mahakamani na wote wamehukumiwa kunyongwa hadi kufa.
Ametaja waliokamatwa na kuhukumiwa na Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora kuwa ni Majuto Lutema (32), Sida Mayeka (47), Kulwa Masunga Senga (44) na Iddy Ramadhani (35) wakazi wa Wilaya ya Sikonge Mkoani Tabora.
Wengine waliotiwa hatiani na Mahakama hiyo na kuhukumiwa kunyongwa ni Mussa Marko (28), Mkazi wa Ushirombo, Wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga na Chandika Fideli (36) Mkazi wa Kijiji cha Mkola, Wilaya ya Urambo.
Aidha katika kuhakikisha jamii inashiriki kikamilifu katika suala zima la ulinzi, Jeshi la Polisi Mkoa wa Tabora limeendelea kutoa elimu kwa jamii katika maeneo yote ya Mkoa huo ili kuimarisha dhana ya Polisi Jamii, mikutano 90,000 ilifanyika.
Aidha vikundi vya ulinzi shirikishi zaidi ya 100 vimeanzishwa na kupewa elimu ili kupunguza uhalifu, na katika kudumisha usalama barabarani wametoa elimu kwa watumiaji wa vyombo vya moto na kuchukuliwa hatua waliovunja sheria.
Kamanda Lulengelule ametoa wito kwa wananchi kujiepusha na vitendo vya uhalifu na kufanya shughuli zilizo halali na kuonya kuwa yeyote atakayeenda kinyume ikiwemo kufanya biashara haramu atachukuliwa hatua kali za kisheria.

Comments
Post a Comment