JESHI LA POLISI LATOA ONYO KALI KWA WANAOHAMASISHA MAANDAMANO NA VURUGU.

 Na Mwandishi Wetu,DmNewsonline

              DODOMA

JESHI  la Polisi Tanzania limetoa onyo kali kwa watu wanaotumia mitandao ya kijamii kuhamasisha vitendo vya uvunjifu wa amani, ikiwemo maandamano yasiyo halali na vurugu. Kupitia taarifa iliyotolewa leo na Msemaji wa Jeshi la Polisi, Makao Makuu Dodoma, jeshi hilo limesema linafuatilia kwa karibu shughuli zote za uhamasishaji huo kwa saa 24.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, awali watu hao walikuwa wakihamasishana kufanya maandamano nchini tarehe 7 Julai. Hata hivyo, ufuatiliaji wa Jeshi la Polisi umebaini kuwa sasa wameondoka kwenye ajenda ya maandamano na kuanza kuhamasisha vitendo vya moja kwa moja vya uhalifu vinavyolenga kuhatarisha usalama wa raia na mali zao.

Miongoni mwa vitendo vilivyotajwa kwenye taarifa hiyo ni kuhamasisha kufunga barabara, kuchoma moto shule ili kusababisha taharuki kwa wazazi, kushambulia wananchi, kukata vichwa, kuua watu, na kuharibu mali za umma na binafsi. Aidha, watu hao wamedaiwa kuhamasishana kuvamia askari wa vyombo vya ulinzi na usalama kwa lengo la kuwapora silaha ili kuzitumia kufanya uhalifu.

Jeshi la Polisi limesisitiza kuwa uhamasishaji wa uhalifu huo chini ya kivuli cha haki ya kufanya maandamano ya amani haukubaliki. Limesema vitendo hivyo ni kinyume cha sheria za nchi, misingi ya utawala wa sheria, pamoja na mikataba ya kikanda na kimataifa, na ni hatari kwa usalama wa nchi.

Kutokana na hali hiyo, Jeshi la Polisi limetangaza kuwa linaendelea kuchukua hatua stahiki dhidi ya watu wote wanaojihusisha na uhamasishaji huo.

 Limetoa wito kwa wananchi kutousambaza ujumbe unaohamasisha uhalifu, bali kuufuta na kutoa taarifa kwa vyombo husika. 

Pia limewahakikishia wananchi kuwa hali ya usalama nchini itaendelea kuwa shwari na italindwa kwa ushirikiano wa karibu baina ya vyombo vya ulinzi na usalama.

Jeshi la Polisi limesema litaendelea kushirikiana na wananchi kubaini, kuzuia na kutanzua vitendo vya uhalifu ili kuhakikisha amani na utulivu vinadumishwa nchini.

Comments

Popular posts from this blog

UONGOZI WA SHIRIKISHO LA VYAMA VYA TIBA ASILI TANZANIA WADAIWA SI HALALI NA UMEKOSA DIRA YA KUENDESHA VYAMA VYA WAGANGA WA TIBA ASILI

MWAKIPOSA ASHINDA NAFASI YA UWENYEKITI WA WENYEVITI WA SERIKALI YA MTAA MKOA WA DAR ES SALAAM

DKT. KIJAZI KUSIMAMIA MIRADI YA MAENDELEO JIMBO LA KOROGWE MJINI.