TIRA: BIMA SI HIARI, NI MGUZO YA KULINDA UCHUMI NA MAISHA YA WANANCHI
Na Mwandishi Wetu, DmNewsTz
Tanga
Meneja wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) Kanda ya Kaskazini, Dkt. Emmanuel Lupilya, amesema kuwa suala la bima si la hiari bali ni nguzo muhimu na injini ya kulinda maisha ya wananchi, shughuli za kilimo, uchumi wa mtu mmoja mmoja pamoja na uchumi wa taifa kwa ujumla.
Dkt. Lupilya ameyasema hayo wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Kifedha yanayoendelea mkoani Tanga kuanzia Januari 19 hadi 26, 2026, alipokuwa akizungumza baada ya Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Mhe. Dadi Kolimba, kutembelea banda la TIRA.
Amesema mamlaka hiyo haitasita kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya makampuni ya bima yatakayokiuka miongozo, sheria na taratibu zilizowekwa, kwani kufanya hivyo kunakwamisha maendeleo ya sekta ya bima na uchumi kwa ujumla.
“Hatutasita kuchukua hatua kali za kisheria kwa makampuni yatakayokiuka miongozo, sheria na taratibu tulizoweka kama mamlaka, kwani kufanya hivyo kunarudisha nyuma maendeleo,” amesema.
Ameeleza kuwa TIRA, kwa kushirikiana na makampuni ya bima, inaendelea kusisitiza utoaji wa elimu ya bima kwa wananchi, akibainisha kuwa Taifa lisipoelimishwa kuhusu bima, serikali italazimika kubeba mzigo mkubwa wa kifedha unaotokana na majanga, umaskini na mdororo wa uchumi.
“Taifa lisipoelimishwa kuhusu bima, ni dhahiri serikali yake itabeba mzigo mkubwa wa kugharamia majengo, athari za umaskini unaojitokeza ghafla, pamoja na mdororo wa uchumi katika mnyororo mzima wa uzalishaji nchini,” amesema.
Ameongeza kuwa uwepo wa TIRA pamoja na makampuni ya bima katika kutoa elimu ya bima ni sehemu muhimu ya kuhakikisha Taifa linaendelea kukuza pato la taifa na kuimarisha ustawi wa wananchi.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa makampuni ya bima kuwa wabunifu katika kubuni bidhaa zao kwa kuzingatia mahitaji halisi ya wananchi, badala ya kutengeneza bidhaa zinazoakisi maslahi ya makampuni pekee.


Comments
Post a Comment