SELF YATOA ELIMU YA MTUMIZI SAHII YA MIKOPO KWA WANANCHI
Na Mwandishi Wetu,DmNewsTz
Meneja Masoko na Uhamasishaji wa Mfuko wa SELF, Linda Mshana, amesema mfuko huo unaendelea kutoa elimu sahihi,kwa wananchi kuhusu matumizi bora ya mikopo, mambo ya kuzingatia kabla ya kuchukua mkopo pamoja na maswali muhimu ya kuuliza Yanayohusiana na taasisi za kifedha, ili kuepuka changamoto ya mikopo ya riba kubwa inayodaiwa kuwanyonya wananchi.
Mshana ameyasema hayo leo Januari 20, 2026, wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Kifedha yanayoendelea katika viwanja vya Usagara, jijini Tanga.
Maadhimisho hayo yalianza Januari 19 na yanatarajiwa kumalizika Januari 26, 2026.
Amesema mfuko wa SELF unawakaribisha wananchi wote wa mkoa wa Tanga kufika katika maadhimisho hayo ili kupata elimu sahihi ya fedha pamoja na kufahamu fursa mbalimbali zilizopo zitakazowawezesha kujiendeleza kiuchumi.
Ameeleza kuwa SELF ina mikopo ya aina mbalimbali ikiwemo mikopo kwa wafanyabiashara wa sekta ya nafaka, wafugaji, wavuvi na wakulima.
Aidha, kuna mikopo ya kuboresha makazi kwa wananchi wanaotaka kuboresha nyumba zao ili zipate muonekano bora zaidi.
“Pia kwa wale wanaotaka kuanzisha au ambao tayari wameanzisha taasisi za kifedha zinazotoa mikopo, na wamepata kibali cha Benki Kuu ya Tanzania (BoT), SELF inatoa fursa ya kuongeza mtaji kupitia mikopo,” amesema.
Mshana amebainisha kuwa swali la riba limekuwa likijitokeza mara kwa mara, jambo linaloonesha kuwa wananchi wengi bado hawana uelewa wa kutosha kuhusu namna sahihi ya kukokotoa riba.
Ameongeza kuwa elimu na mafunzo kuhusu masuala hayo hutolewa kupitia mfuko huo ili kuwajengea wananchi uelewa mpana wa masuala ya kifedha.
Amesema SELF ni taasisi iliyo chini ya Wizara ya Fedha, inayojikita katika kuhamasisha wananchi kufanya kazi kwa bidii na kujikwamua kiuchumi kupitia mikopo yenye masharti nafuu, sambamba na kutoa elimu ya fedha na bima.


Comments
Post a Comment