NEEMA YAWASHUKIA WAKULIMA WA TUMBAKU TABORA

  Na Allan Kitwe,DmNewsonline

                   TABORA 

SERIKALI ya awamu ya 6 inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imepongezwa kwa kupanua wigo wa soko la zao la tumbaku hali ambayo imechochea wakulima kuongeza uzalishaji na kuwa na uhakika wa masoko.

Pongezi hizo zimetolewa na Meneja Mkuu wa WETCU 2018 Ltd Samwel Jokeya alipokuwa akizungumza  na Mwandishi wa mndao huu wa DmNewsonline  aliyetaka kujua mafanikio ya wakulima wa tumbaku wa Mkoa huo katika miaka 4 ya Rais Samia.

Amesema kuwa changamoto za wakulima wa tumbaku katika miaka 4 ya uongozi wake zimepungua sana na masoko ya zao hilo na mazao mengine sasa ni ya uhakika tofauti na miaka mingine, na tumbaku yote inayozalishwa sasa inauzwa.

 ‘Hadi sasa tuna jumla ya makampuni 21 nchini yaliyoidhinishwa kununua zao la tumbaku yakiwemo ya wazawa, hali hii imeongeza ushindani wa bei, wengine wanalipa hadi dola 3 kwa kilo, hiki ndicho wanachotaka wakulima wetu’, amesema 

Jokeya amepongeza serikali kupitia Bodi ya Tumbaku (TTB) na Waziri mwenye dhamana kwa kusimamia vizuri kilimo cha zao hilo na suala zima la masoko hali ambayo imeleta neema kubwa kwa wakulima ikiwemo kujiongezea kipato.

Serikali ya awamu ya 6 haitaki ubabaishaji kwenye malipo ya wakulima, hivyo akaonya kuwa kampuni yoyote itakayochelewesha au kudhulumu fedha za wakulima itachukuliwa hatua kali za kisheria na itafungiwa kununua zao hilo.

Naye Mrajisi wa Mkoa wa Tabora Venance Msafiri amefafanua kuwa ili kukomesha wizi au dhuluma kwa wakulima serikali imeelekeza kila mkulima aingiziwe fedha zake kwenye akaunti yake moja kwa moja na sio kupitia vyama vyao.

Amebainisha kuwa hii itasaidia kumaliza malalamiko ya baadhi ya wakulima kukatwa fedha zao kinyume na utaratibu ikiwemo kubambikiziwa madeni ambayo hayawahusu.

 Msafiri ametoa wito kwa kampuni zote zilizoruhusiwa kununua tumbaku msimu huu kuiga mfano wa kampuni ya Mkwawa ambayo imekuwa kinara wa kununua na kulipa wakulima kwa wakati na huu ndio uzalendo wa kweli. 

Comments

Popular posts from this blog

UONGOZI WA SHIRIKISHO LA VYAMA VYA TIBA ASILI TANZANIA WADAIWA SI HALALI NA UMEKOSA DIRA YA KUENDESHA VYAMA VYA WAGANGA WA TIBA ASILI

MWAKIPOSA ASHINDA NAFASI YA UWENYEKITI WA WENYEVITI WA SERIKALI YA MTAA MKOA WA DAR ES SALAAM

KILINDI BARABARA BADO NI CHANGAMOTO