WANAWAKE TABORA WAHAMASISHWA KUWANIA UBUNGE, UDIWANI





Na Allan Kitwe, DmNewsonline

              TABORA 

ZIKIWA zimebakia siku 123 sawa na miezi 4 kabla ya kufanyika uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani hapa nchini, Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Mkoani Tabora umewataka wanawake wote wenye sifa kujitokeza kwa wingi kuchukua fomu.

Wito huo umetolewa jana na Katibu wa Jumuiya hiyo ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoani hapa Rhoda John Madaha alipokuwa akiongea na mwandishi wa gazeti hili ofisini kwake.

Amesema kuwa akinamama wana vipaji vingi na uwezo mkubwa wa kuongoza, hivyo anatamani kuona wanawake wengi zaidi mwaka huu wakijitokeza kuchukua fomu punde tu dirisha la utoaji fomu litakapofunguliwa.

Rhoda amebainisha nafasi ambazo wanawake wa Tanzania Bara wanaweza kugombea katika uchaguzi huo kuwa ni ubunge wa jimbo, ubunge wa viti maalumu, udiwani wa kata na udiwani wa viti maalumu.

‘Hii ni fursa muhimu sana, naomba akinamama wote wa Mkoa wa Tabora wenye nia, uwezo na sifa zinazotakiwa waje kuchukua fomu za ubunge na udiwani, msikubali kukatishwa tamaa na mtu yeyote, tunataka ’, amesema.    

Katibu ameeleza kuwa kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa ndani ya Chama, zoezi la uchukuaji na urejeshaji fomu za kuomba kuwania nafasi hizo litaanza Juni 28 mwaka huu saa 2 asubuhi na kuhitimishwa Julai 2 mwaka huu saa 10 alasiri.

Amesisitiza kuwa Chama Cha Mapinduzi ni chama cha kidemokrasia, hivyo mchakato wa kupata wagombea ndani ya chama hicho haubagui mtu, kila mmoja anaweza kuteuliwa na kuchaguliwa katika nafasi yoyote.

Ametoa wito kwa wanawake wote kutoka Wilaya zote 7 za Mkoa huo za Sikonge, Urambo, Kaliua, Nzega, Igunga, Uyui na Manispaa Tabora kujitokeza kwa wingi kuchukua fomu ili kuomba nafasi za udiwani au ubunge.

Rhoda amepongeza uamuzi wa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM kupitisha jina la Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea pekee wa kiti cha Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika uchaguzi huo na Dkt Emanuel Nchimbi kuwa mgombea mwenza.   




Comments

Popular posts from this blog

UONGOZI WA SHIRIKISHO LA VYAMA VYA TIBA ASILI TANZANIA WADAIWA SI HALALI NA UMEKOSA DIRA YA KUENDESHA VYAMA VYA WAGANGA WA TIBA ASILI

MWAKIPOSA ASHINDA NAFASI YA UWENYEKITI WA WENYEVITI WA SERIKALI YA MTAA MKOA WA DAR ES SALAAM

KILINDI BARABARA BADO NI CHANGAMOTO