TAKUKURU YAPAISHA MAPATO PWANI
Na Mwandishi wetu,DmNewsonline
Na Gustaphu Haule, Pwani
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Pwani imeshiriki katika kupaisha makusanyo ya mapato ya Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha na kufikia kiasi cha zaidi ya Sh.bilioni 1.6.
Fedha hizo ni makusanyo ya ushuru katika kipindi cha miezi mitatu ikiwa ni kuanzia Januari hadi Machi ambapo Takukuru ilifanya uzuiaji katika ukusanyaji wa mapato upande wa ushuru wa huduma.
Naibu Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Pwani Ezekia Sinkala,ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na Waandishi wa habari katika mkutano uliofanyika Mei 15/2026 ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa utendaji kazi katika kipindi cha Januari hadi Machi 2026.
Sinkala ,amesema kuwa fedha hizo zilikuwa zinapotea kutokana na baadhi ya wafanyabiashara kufuta stakabadhi za mauzo na kutokuwa tayari kulipa ushuru wa huduma .
Aidha,Sinkala amesema kuwa katika ufuatiliaji huo Takukuru Mkoa wa Pwani ilibaini mambo mbalimbali ikiwemo wafanyabiashara kufuta stakabadhi za mauzo ambazo zilishafanyika na hivyo kushusha jumla ya mauzo.
Amesema jambo lingine walilolibaini ni baadhi ya wafanyabiashara kufanya biashara bila kutoa risiti za EFD hususani maduka ya vifaa vya ujenzi,maduka ya jumla na bidhaa zitokazo viwandani pamoja na uhamishaji wa bei za bidhaa kutoka kampuni mama kwenda kwenye matawi yake kwa lengo la kupunguza mauzo.
Amesema Takukuru imesaidia kuongeza Makusanyo hayo kwa kushirikiana na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha Dkt.Rogers Shemwelekwa katika kukusanya mapato ya Manispaa katika robo tatu mfululizo.
Sinkala ,amesema kuwa robo ya kwanza ilikusanywa zaidi ya Sh.bilioni 1.5 na robo ya pili ilikusanywa zaidi ya Sh. bilioni 1.8 huku ya robo ya tatu ilikusanywa zaidi ya Sh.bilioni 1.6 japo zoezi katika robo ya tatu linaendelea na kufanya jumla ya makusanyo kufikia zaidi ya Sh.bilioni 4.9.
"Katika robo tatu mfululizo Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha kwa kushirikiana na Takukuru Mkoa wa Pwani kumekuwa na mafanikio makubwa ya ukusanyaji wa mapato kwani hadi sasa zimekusanywa zaidi ya Sh.bilioni 4.9 fedha ambazo zilikuwa zinapotea kwasababu mbalimbali," amesema Sinkala.
Sinkala katika hatua nyingine amesema katika Wilaya ya Kibiti Takukuru imewezesha kuokoa na kurudishwa kwa mifuko ya saruji 30 yenye thamani ya Sh.570,000 iliyotolewa stoo kinyume na utaratibu katika ukaguzi uliofanywa kwenye mradi wa ujenzi wa kituo cha afya Nyamisati.
Amesema mifuko hiyo ilionekana kutolewa stoo na wahusika lakini haikuombwa wala kukabidhiwa kwa fundi lakini baada ya ukaguzi walielekezwa wahusika kurudisha saruji hiyo ili mradi uendelee kwa kiwango na ubora huku hatua zingine za kuhusu suala hilo zikiendelea .
Kuhusu ufuatiliaji wa matumizi ya fedha za utekelezaji wa miradi ya maendeleo Sinkala amesema Takukuru Mkoa wa Pwani imefanikiwa kufuatilia matumizi ya fedha za utekelezaji wa miradi ya maendeleo 55 yenye thamani zaidi ya Sh.bilioni 10.1.
Amesema katika ufuatiliaji huo Takukuru ilishauri mapungufu yaliyojitokeza kwenye baadhi ya miradi hiyo hususani katika sekta ya Elimu,Afya,Maji na Barabara ambapo ufuatiliaji huo umesaidia kuwa na miradi bora yenye kuendana na matumizi ya fedha zilizotolewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi husika.
Sinkala amesema katika kipindi hicho cha Januari hadi Machi 2026 Takukuru Mkoa wa Pwani imefanya uchambuzi wa mifumo 14 na warsha 3 zinazohusu utoaji wa huduma bora za afya kwa makundi maalum ya watoto,huduma za watu wanaoishi na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi,walemavu na wazee lengo ni kuhakikisha makundi hayo yanapata huduma bila shida yoyote.
Amesema chambuzi hizo zilipelekea kuwekeana maazimio ya kurekebisha mapungufu yaliyobainika wakati wa kufanya uchambuzi na maazimio hayo yaliwekwa na wadau kwa kushirikiana na Takukuru.
Sinkala ametaja maazimio hayo ambapo ni pamoja na kuwa na mafunzo endelevu kwa watoa huduma wote kuhusu namna ya kuwahudumia vizuri wagonjwa wenye mahitaji maalum ambayo yatasaidia kuondoa mianya ya rushwa.
Amesema maadhimisho mengine ni kuboresha vyoo vya wagonjwa wenye mahitaji maalum kulingana na mahitaji ya wagonjwa pamoja na kuongeza faragha katika utoaji wa huduma za watu wanaoishi na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi tofauti na ilivyokuwa wanahudumiwa mwanzo.
Kuhusu uchunguzi mashtaka Sinkala amesema kuwa katika kipindi hicho Takukuru imepokea taarifa 71 ambapo 18 hazikuhusu vitendo vya rushwa na taarifa 53 zilihusu vitendo vya rushwa na hadi sasa zinashughulikiwa na zipo katika hatua mbalimbali.
Amesema Wananchi wamekuwa wazalendo kwa kufika na kutoa ushahidi Mahakamani katika kesi za makosa ya rushwa yaliyofanyiwa uchunguzi na kwamba hiyo imesaidia Takukuru kumaliza jumla ya kesi 7ambapo kesi 5 Jamhuri ilishinda ,kesi mpya 3 zilifunguliwa na kesi 14 zinaendelea Mahakamani.
Hatahivyo, Sinkala ametoa wito kwa Wananchi, watumishi na wadau wote kuendelea kuungana mkono jitihada za mapambano dhidi ya rushwa ,kufichua wote walioshiriki kufanya vitendo vya rushwa kwa kutoa taarifa sahihi zitakazowezesha kuwachukulia hatua wahusika kupitia namba 113 ya bila malipo. 




Comments
Post a Comment