JOWUTA YAZITAKA TAASISI,WAMILIKI WA VYOMBO VYA HABARI KUWAANDIKISHA WANAHABARI WCF
Na mwandishi wetu,DmNewsTz
Dar es salaam
Chama cha Wafanyakazi katika Vyombo vya Habari Tanzania (JOWUTA) kimezitaka taasisi na wamiliki wa vyombo vya habari nchini kuhakikisha wanawaandikisha wanahabari katika Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) pamoja na kuwapatia ajira zenye mikataba rasmi ili waweze kunufaika na haki na stahiki zao za msingi kazini.
Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa mafunzo kuhusu fidia kwa wafanyakazi kwa wanachama wa JOWUTA, Mwenyekiti wa chama hicho, Mussa Juma Siwayombe amesema bado wanahabari wengi nchini wanafanya kazi bila ajira za kudumu wala mikataba, hali inayowanyima fursa ya kupata huduma muhimu za hifadhi ya jamii na fidia wanapopatwa na madhara yatokanayo na kazi zao.
Amesema zaidi ya asilimia 70 ya wanahabari nchini hawana ajira rasmi jambo ambalo ni changamoto kubwa kwa ustawi wao na tasnia ya habari kwa ujumla, huku akisisitiza umuhimu wa umoja na mshikamano wa wafanyakazi katika kudai haki zao.
Siwayombe amesema mafunzo hayo yaliyoandaliwa kwa kushirikiana na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) yataongeza uelewa kwa wanahabari kuhusu mafao na huduma zinazotolewa na mfuko huo, hatua ambayo itasaidia pia kuelimisha jamii kupitia habari zitakazoandikwa na wanahabari hao.
Aidha, ameushukuru uongozi wa WCF chini ya Mkurugenzi Mkuu Dkt. John Mduma kwa kuwezesha kufanyika kwa mafunzo hayo kwa wanachama wa JOWUTA kutoka mikoa ya Dar es Salaam na Pwani, akisema mafunzo hayo ni mwanzo wa programu ya kuwafikia wanachama wa chama hicho katika kanda nyingine nchini ikiwemo Kanda ya Ziwa, Kaskazini na Nyanda za Juu Kusini.
Katika hotuba yake, Siwayombe amesema mafunzo hayo pia yanaimarisha mahusiano kati ya WCF, vyama vya wafanyakazi vilivyo chini ya TUCTA pamoja na vyombo vya habari nchini.
Amesema Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi ni taasisi muhimu kwa wafanyakazi kwani umeanzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi kwa lengo la kutoa fidia kwa wafanyakazi wa sekta binafsi na umma wanaopata madhara, magonjwa au vifo vitokanavyo na kazi zao.
Pia amewataka washiriki wa mafunzo hayo kutumia elimu watakayoipata kuwa mabalozi wa kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa huduma zinazotolewa na WCF pamoja na taratibu za kupata fidia.
Sambamba na hilo, Siwayombe ameipongeza Serikali kwa jitihada zake za kushughulikia changamoto za wanahabari nchini, akieleza kuwa tayari kumekuwa na mazungumzo kati ya viongozi wa JOWUTA na Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Wizara ya Kazi pamoja na Kamishna wa Kazi kuhusu waajiri wanaowatumia wanahabari bila mikataba rasmi ya ajira.
Amesema katika siku za hivi karibuni Serikali inatarajiwa kuanza msako maalumu katika vyombo vya habari ili kubaini waajiri wanaokiuka sheria za kazi kwa kutowaajiri rasmi wanahabari.
Akihitimisha hotuba yake, Siwayombe amewakumbusha wafanyakazi umuhimu wa mshikamano kupitia kauli mbiu ya wafanyakazi duniani ya “Solidarity Forever”, akisema umoja ni msingi muhimu katika mapambano ya kutetea haki na maslahi ya wafanyakazi.













Comments
Post a Comment