ATE YABORESHA TUZO ZA MWAJIRI BORA 2026 KWA MFUMO MPYA WA UWAZI NA USHIRIKISHWAJI
Na mwandishi wetu,DmNewsTz
Dar es salaam
Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), Adv. Suzanne Ndomba-Doran amesema Tuzo za Mwajiri Bora wa Mwaka 2026 (EYA) zimeboreshwa kwa mfumo mpya unaolenga kuongeza uwazi, ushirikishwaji na kuendana na mabadiliko ya dunia ya ajira.
Akizungumza wakati wa uzinduzi rasmi wa tuzo hizo, Adv. Ndomba-Doran alisema EYA imekuwa nguzo muhimu katika sekta ya ajira nchini kwa zaidi ya miaka 20 kwa kutambua taasisi zinazowekeza katika ustawi wa wafanyakazi, mazingira bora ya kazi na maadili ya biashara.
“Leo si uzinduzi wa kawaida. Leo tunaandika ukurasa mpya katika historia ya EYA,” alisema.
Alisema mwaka uliopita ATE ilisimamisha kwa muda utoaji wa tuzo hizo ili kufanya mapitio ya kina na kuhakikisha mfumo wake unaendana na mahitaji ya sasa ya waajiri na wafanyakazi.
Kwa mujibu wa Adv. Ndomba-Doran, mapitio hayo yalihusisha wadau mbalimbali wakiwemo wanachama wa ATE, wataalamu na washauri wa sekta ya ajira, ambapo walipokea maoni yaliyotaka EYA iwe wazi zaidi, jumuishi na yenye mchango wa muda mrefu kwa waajiri.
“Wadau walituambia wazi kwamba EYA inahitaji kubadilika, iwe rahisi kueleweka, iwe jumuishi zaidi na isiwe tukio la usiku mmoja wa utoaji tuzo pekee, bali iwe chombo cha kujifunza na kuboresha utendaji mwaka mzima,” alisema.
Alieleza kuwa mapema mwezi Mei mwaka huu, ATE ilifanya warsha maalum katika Hoteli ya Four Points by Sheraton jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuthibitisha mapendekezo ya maboresho ya mfumo wa EYA.
Adv. Ndomba-Doran alisema baadhi ya mapendekezo yaliyopokelewa ni pamoja na kuifanya EYA kuwa chapa maalum ya kitaifa, kuanzishwa kwa tovuti maalum ya EYA, kuanzishwa kwa tuzo za kisekta pamoja na kuboresha vigezo vya tathmini na matumizi ya wataalamu wenye weledi katika ukaguzi.
Alisema mfumo mpya wa EYA sasa utaangalia maeneo mbalimbali ikiwemo uongozi na utawala, utamaduni wa shirika, usawa na ujumuishaji, maendeleo ya wafanyakazi, matumizi ya teknolojia katika HR, afya na usalama mahali pa kazi pamoja na ubunifu na tija.
Aidha, alisema kwa mara ya kwanza EYA itaanzisha tuzo za kisekta ili kutoa ushindani wenye haki kwa taasisi zinazotoka katika sekta tofauti.
“Hii italeta uhalisia zaidi kwa sababu haiwezekani kulinganisha taasisi kubwa za kimataifa na biashara ndogo au sekta tofauti kabisa,” alisema.
Katika hatua nyingine, Adv. Ndomba-Doran alisema mfumo huo mpya umeongeza ushirikishwaji kwa SMEs pamoja na sekta isiyo rasmi, huku makundi mapya yakianzishwa ikiwemo SME Iliyoboreshwa Zaidi, Mwajiri Chipukizi wa Mwaka na Ubunifu Bora wa HR kwa SMEs.
Alisema sekta isiyo rasmi sasa itatambuliwa rasmi katika EYA kwa kuangalia mchango wake katika ustawi wa wafanyakazi, maadili ya kazi, ubunifu na mchango kwa jamii.
Kuhusu uwazi wa mchakato wa tathmini, alisema kutakuwa na tathmini huru za kitaalamu, ushirikishwaji wa wafanyakazi kupitia tafiti, ukaguzi wa mazingira ya kazi pamoja na maamuzi yatakayofanywa na jopo huru.
“Kila alama itakuwa na ushahidi na kila ushindi utajengwa juu ya ukweli,” alisema.
Aidha, alisema EYA sasa haitakuwa tukio la utoaji tuzo pekee bali safari ya mwaka mzima ya kujifunza, kubadilishana uzoefu na kuboresha mazingira ya kazi nchini.
Kwa upande wake, Mshauri elekezi kutoka Auditax International Dkt. Straton Makundi alisema usajili wa washiriki wa Tuzo za Mwajiri Bora wa Mwaka 2026 utafanyika kwa njia ya mtandao ili kurahisisha upatikanaji wa huduma hiyo kwa waajiri kutoka maeneo mbalimbali nchini.
Alisema matumizi ya mfumo wa kidijitali yataongeza uwazi, kasi na ufanisi katika mchakato mzima wa usajili na tathmini sambamba na kuendana na mabadiliko ya teknolojia katika dunia ya sasa ya ajira.
“Tunataka kila mwajiri aweze kushiriki bila vikwazo vya umbali au gharama kubwa za usafiri. Mfumo wa online utatoa nafasi sawa kwa taasisi kubwa, ndogo na hata sekta zisizo rasmi kushiriki kikamilifu,” alisema Dkt. Makundi.







Comments
Post a Comment