WAZIRI NCHENGERWA :ATAKAYESHINDWA KUENDANA NA KASI ILIYOPO ATAONDOLEWA

Waziri wa Afya Mohamed Mchengerwa ( aliyevaa kofia) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa boti mpya ya kisasa kwa ajili ya kutolea huduma ya chanjo kwa watoto waishio maeneo ya visiwani katika Halmashauri ya Kibiti Mkoa wa Pwani,hafla ya uzinduzi huo ilifanyika Aprili 29/2026 katika Bandari ya Nyamisati


Na Gustaphu Haule,DmNewsonline

             PWANI

WAZIRI wa Afya Mohamed Mchengerwa amesema kiongozi wa ambaye atasababisha kutokuwepo na dawa na vifaa tiba katika vituo vya kutolea huduma za afya vilivyopo katika eneo lake anatakiwa kujitathmini na endapo atashindwa kuendana na kasi iliyopo ataondolewa katika nafasi yake.

Mchengerwa amewataja viongozi hao kuwa ni pamoja na Waganga wafawidhi wa Wilaya na timu zao, Waganga wafawidhi wa Mikoa na timu zao pamoja na Waganga wakuu wa Wilaya na Waganga wakuu wa Mikoa.

Mchengerwa amesisitiza kwa mamlaka zote za sekta ya afya wakiwemo Waganga wakuu wa Mikoa na Wilaya kuhakikisha hakuna mgonjwa anayekosa dawa pale ambapo anakwenda hospitali kupata matibabu.

Amesema akisikia popote nchini mgonjwa amekwenda hospitali halafu akakosa dawa ni wazi kuwa viongozi wa eneo hilo kuanzia Mganga Mkuu wa Wilaya hadi Mganga Mfawidhi wote atawaondoa.

Mchengerwa ametoa kauli hiyo Aprili 29/2026 wakati akizungumza na Wananchi, viongozi mbalimbali wa Serikali na watumishi wa kada ya afya katika maadhimisho ya Wiki ya Afya yaliyofanyika katika viwanja vya Shule ya Sekondari Zimbwini iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti Mkoa wa Pwani.

Amesema kuwa yeye hatokubali kuona mwananchi anakosa dawa kwakuwa yapo mambo ya kufanyia mzaha lakini sio jambo la dawa na atakuwa mkorofi kwa mtumishi ambaye atasababisha mgonjwa kukosa dawa hospitalini.

Amesema tayari walikaa katika vikao vyao na kukubaliana suala la dawa na ikaelezwa kuwa dawa zipo za kutosha na hakuna sababu ya mgonjwa kukosa na dawa na Mganga Mkuu wa Serikali Grace Maghembe alishusha maagizo hayo ngazi zote za chini.

Amesema hakuna sababu ya Mtanzania wa eneo lolote nchini kukosa dawa wakati zipo za kutosha kama ambavyo takwimu zinasema kuwa dawa zipo kwa asilimia 90 na takwimu hizo zimetolewa na wataalamu wenyewe sasa ikitokea vinginevyo mhusika atachukuliwa hatua.

Mchengerwa ameongeza kuwa anatambua  utegemezi wa dawa kutoka nje ya nchi ni changamoto lakini Serikali inatekeleza mkakati madhubuti wa kuongeza upatikanaji wa dawa ndani ya nchi.

Amesema Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan imekuta uzalishaji wa dawa nchini upo kwa  asilimia 16 lakini inawezekana Taifa likazalisha dawa zake lenyewe.

Amesema kutokana na malengo ya Serikali ya awamu ya sita tayari wapo katika kutekeleza mpango wa uzalishaji dawa na sasa Mei 08/2026 utasainiwa mkataba mkubwa wa kujenga viwanda vya kuzalisha dawa nchini .

Amesema mkataba huo utafanyika katika hospitali ya  Mloganzila ambapo makampuni makubwa 60 duniani yameonesha nia ya kuzalisha dawa mpango ambao utaitoa Tanzania kutoka kuzalisha dawa kwa asilimia 16 hadi kufika asilimia 80 ya mwaka 2030.

"Tunapokwenda 2030 wakati Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan anakwenda kukamilisha awamu yake ya pili ya uongozi wake Wizara itahakikisha inamuheshimisha Rais Samia kwa kuzalisha dawa asilimia 80 ,"amesema Mchengerwa 

Aidha, Mchengerwa amesema kuwa ongezeko la viwanda vya kuzalisha dawa nchini itasaidia kuondoka utegemezi wa mataifa ya nje,kuokoa fedha za kigeni,na hata kuongeza ajira kwa Watanzania.

Kuhusu kuimarisha huduma ya chanjo kwa watoto wadogo nchini Mchengerwa amesema Wizara ya afya imejipanga kikamilifu na kupitia wadau wake tayari Serikali imenunua boti 7 kwa ajili ya kusaidia kutoa chanjo kwa watoto waishio maeneo ya visiwani.

Mganga Mkuu wa Serikali Grace Maghembe amesema kuwa maadhimisho ya Wiki ya Afya yalianza mwaka 2025 ikiwa ni sehemu ya kufanyia tathmini ya utoaji wa huduma za afya nchini.

Maghembe amesema kuwa maadhimisho ya mwaka huu Wizara ya afya  imefanya shughuli mbalimbali ikiwemo kufanya shughuli za usafi wa mazingira na kudhibiti magonjwa mbalimbali .

Amesema huduma zilizotolewa ni pamoja na kutoa huduma za chanjo kwa kutumia Kliniki tembezi,huduma za Mkoba zilizowafikia Wananchi 8600,kutoa elimu ya chanjo kupitia vyombo vya habari, usimamizi shirikishi ngazi za jamii,na makabidhiano ya boti 7 kwa ajili ya kutolea huduma ya chanjo kwa watoto hususani waishio visiwani.

Amesema katika kuhimiza usafi wa mazingira nchini Wizara ilikuwa ikiendesha suala la usafi wa mazingira kote nchini chini ya utekelezaji wa kauli mbiu ya Mtu ni Afya.

Amesema mwaka 2026 suala la usafi wa mazingira lilikuwa katika mashindano maalum yaliyofanyika kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza ilikuwa ni katika Manispaa,Majiji,Miji ,Wilaya  hadi Mitaa lakini awamu ya pili ni kwa Halmashauri zote 184  katika upande wa Shule za Msingi na Sekondari,sekta binafsi,hospitali za Wilaya ,na vyuo vikuu ambapo kila  eneo lilitoa mshindi wa kwanza,wapili na watatu.

Akizungumza kuhusu boti za kutolewa chanjo kwa watoto Maghembe amesema kuwa boti hizo Saba zimenunuliwa kwa gharama ya Sh.bilioni 1.1 na zitasaidia katika maeneo ya visiwani ambayo watoto wa maeneo hayo walikosa kupata huduma hiyo ya chanjo.

Maghembe amesema boti hizo zimekwenda katika Wilaya ya Kigoma Vijijini, Ukerewe, Nkasi, Uvinza, Kibiti na boti mbili zimekwenda Zanzibar ambapo kazi yake kubwa ni kuhamasisha masuala mbalimbali ya afya kwa watoto wadogo na Wananchi ambapo matarajio yake ni kuhakikisha kila mtoto anafikiwa kwa wakati.

Kwa upande wake mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Bunge ,Huduma za Afya na Ukimwi Johanes Lukumay ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Arumeru Magharibi amemshukuru Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa aliohufanya katika sekta ya afya .

Lukumay amesema Serikali imeweka Sheria ya mwaka 2023 kuhakikisha suala la  bima ya afya kwa wote unatekelezwa kwa Watanzania wote na huduma hiyo inaangalia magonjwa yote .

Hatahivyo,amesema bima ya afya kwa wote inashughulikia magonjwa yote na sasa imeanza kutekelezwa kwa kuanza na watu wanaoishi katika kaya maskini na Serikali tayari imetoa Sh.bilioni 48 kutekeleza mpango huo. Waziri wa Afya Mohamed Mchengerwa ( aliyevaa kofia) akitoa chanjo ya matone kwa watoto katika maadhimisho ya Wiki ya Afya yaliyofanyika katika viwanja vya Shule ya Sekondari Zimbwini iliyopo katika Halmashauri ya Kibiti Mkoani Pwani Aprili 29/2026 
  Mganga Mkuu wa Serikali Grace Maghembe ( kushoto) akitoa chanjo ya matone kwa mtoto ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Afya Kitaifa yaliyofanyika Aprili 26/2026 katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti Mkoani Pwani
 Wananchi wa Kibiti wakishiriki maadhimisho ya Wiki ya Afya Kitaifa yaliyofanyika Aprili 29/2026 katika viwanja vya Shule ya Sekondari Zimbwini
Maadhimisho ya Wiki ya Afya Kitaifa yaliyofanyika katika viwanja vya Shule ya Sekondari Zimbwini Wilayani Kibiti Mkoa wa Pwani Aprili 29/2026
 Mganga Mkuu wa Serikali Grace Maghembe ( Kulia) akimshuhudia  Waziri wa Afya Mohamed Mchengerwa ( katikati mwenye kofia) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa boti mpya ya kutolea huduma ya chanjo kwa watoto wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti wanaoishi katika maeneo ya visiwani,hafla hiyo ilifanyika Aprili 29/2026 katika Bandari ya Nyamisati iliyopo Kibiti Mkoani Pwani

Comments

Popular posts from this blog

UONGOZI WA SHIRIKISHO LA VYAMA VYA TIBA ASILI TANZANIA WADAIWA SI HALALI NA UMEKOSA DIRA YA KUENDESHA VYAMA VYA WAGANGA WA TIBA ASILI

DKT. KIJAZI KUSIMAMIA MIRADI YA MAENDELEO JIMBO LA KOROGWE MJINI.