VIJANA ZAIDI YA 60 WALIOHITIMU FDC NZEGA WAPATA AJIRA
Na Allan Kitwe, DmNewsonline
NZEGA
TAASISI, Mashirika ya Umma na makampuni binafsi yamepongezwa kwa kutoa fursa za ajira kwa vijana wa kike na kiume wanaohitimu mafunzo ya ufundi katika fani mbalimbali kwenye Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi (FDC) .
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Chuo Cha Maendeleo ya Wananchi Nzega (Nzega FDC) Nichodemus Shirima alipokuwa akiongea na waandishi wa habari waliomtembelea Ofisini kwake jana ili kujionea maendeleo ya chuo hicho.
Ameshukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuvifanyia maboresho makubwa vyuo vyote vya maendeleo ya wananchi nchini na kuvipatia vifaa vya kutosha vya kufundishia na kujifunzia hali ambayo imechochea vyuo hivyo kutoa elimu bora.
‘Zaidi ya vijana sitini (60) waliohitimu fani mbalimbali katika chuo chetu hapa Nzega wamepata ajira rasmi katika taasisi mbalimbali za umma na makampuni ya watu binafsi na wengine wamejiajiri na wanapata kipato cha uhakika’, ameeleza.
Shirima amefafanua vijana walioajiriwa kuwa ni wa fani za ufundi bomba (zaidi ya 20) huku zaidi ya 30 wakijiajiri katika fani hiyo, umeme (zaidi ya 15 wameajiriwa) na ufundi magari ( zaidi ya vijana 15), ushonaji na ubunifu mavazi (zaidi ya 25).
Amebainisha kuwa mafunzo yanayotolewa katika vyuo hivyo ni ya uhakika na yanawajengea uwezo wa kufanya kazi mahali popote pale katika fani zao, na hii hupelekea taasisi, mashirika na makampuni binafsi kuvutiwa nao.
‘Tumejiwekea utaratibu wa kufuatilia vijana wanaohitimu katika chuo chetu, ili kujua wanaendeleaje na wanafanya nini huko waliko, na wale wote waliopata ajira rasmi na zisizo rasmi tuna taarifa zao’, ameongeza.
Shirima amedokeza kuwa chuo hicho kimeendelea kupokea vijana wengi zaidi wanaokuja kusoma fani mbalimbali kutokana na kuboreshwa miundombinu na uwepo wa vifaa vya kutosha vya kufundishia, na mazoezi ya kutosha ya vitendo. 






Comments
Post a Comment