KUNDI LA 11 LAMPANGO WA FFP LAKABIDHI HUNDI YA MILIONI 30 KWA JKCI
Na mwandishi wetu,DmNewsTz
Dar es salaam
Kundi la 11 la Mpango wa Female Future Programme (FFP) limekabidhi hundi ya shilingi milioni 30 kwa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete Cardiac Institute (JKCI) kwa ajili ya kusaidia watoto wanaokabiliwa na matatizo ya moyo.
Mchango huo umetolewa kama sehemu ya shughuli za Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) za darasa la washiriki 162 wa mwaka 2025, ambalo ni darasa kubwa zaidi kuwahi kushiriki katika historia ya mpango huo unaoratibiwa na Association of Tanzania Employers (ATE).
Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano, Mtendaji Mkuu wa ATE, Bi. Suzanne Ndomba-Doran, amesema kuwa Mpango wa Female Future Programme haujikita tu katika utoaji wa mafunzo bali pia unalenga kuwajengea wanawake viongozi uwezo wa kuchukua hatua chanya katika jamii. Alisema hadi sasa jumla ya wanawake 620 wamehitimu kupitia mpango huo.
Alifafanua kuwa utekelezaji wa mradi wa CSR ni sehemu ya mafunzo ya kukuza ujuzi wa uongozi wa juu ambayo washiriki wa Kundi la 11 wamepata. Mpango huo ulianzishwa nchini Norway takribani miaka 15 iliyopita kupitia taasisi dada ya ATE, Confederation of Norwegian Enterprise (NHO), na ulizinduliwa rasmi nchini mwaka 2016 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, ambaye wakati huo alikuwa Makamu wa Rais.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dkt. Peter Richard Kisenge, amesema taasisi hiyo ina matawi saba na hufanya wastani wa upasuaji 800 kwa mwaka, huku kiwango cha vifo kikiwa chini ya asilimia tatu. Ameongeza kuwa asilimia 50 ya timu ya menejimenti ya taasisi hiyo ni wanawake.
Rais wa darasa la Kundi la 11, Mhandisi Esther Christopher Mwavumilo, amesema wameguswa na hali ya watoto wanaohitaji upasuaji wa moyo, hasa kutokana na gharama kubwa ya matibabu inayofikia wastani wa shilingi milioni nane kwa mtoto mmoja. Amesema kama viongozi, wameona ni wajibu wao kuchangia na kutoa wito kwa wadau wengine kuunga mkono jitihada hizo.
Naye Mtendaji Mkuu wa Heart Team Africa Foundation (HTAF), Dkt. Naihizijwa Majini, amesema mchango huo utasaidia kwa kiasi kikubwa kuendeleza matibabu kwa watoto wenye matatizo ya moyo na kuhimiza wanawake mameneja kujitokeza kujiunga na Mpango wa Female Future Programme.












Comments
Post a Comment