VIKUNDI 222 UYUI VYAWEZESHWA MIKOPO NAFUU YA BILIONI 1

      Na Allan Kitwe,DmNewsonline

                  TABORA 

HALMASHAURI ya Wilaya ya Uyui Mkoani Tabora imetoa mikopo nafuu isiyo na riba ya shilingi bilioni 1 kwa vikundi 222 vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu wanaojishughulisha na biashara ndogo ndogo ili kuwainua kiuchumi.

Akizungumza kwenye hafla fupi ya kukabidhi mfano wa hundi za mikopo hiyo jana, Afisa Maendeleo ya Jamii wa Wilaya hiyo Amoniche Mtweve amesema kuwa mikopo hiyo imetokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri.

Ameongeza kuwa jumla ya wanachama 1,121 wanaounda vikundi hivyo wamenufaika na mikopo hiyo na kuwapa nguvu ya kuendeleza miradi yao ya biashara na uzalishaji mali katika maeneo yao.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Shabani Katalambula, amewataka wanufaika kurejesha mikopo hiyo kwa wakati ili kuwezesha wananchi wengine kunufaika na mikopo hiyo katika awamu zijazo.

Amefafanua lengo la mikopo hiyo kuwa ni kusaidia vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kujikwamua kiuchumi kupitia miradi midogo midogo ya ujasiriamali wanayoifanya hivyo akawataka kuitumia kwa lengo lilokusudiwa.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Uyui, Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Neema Mfugale, amewataka kuwa na nidhamu ya matumizi ya fedha hizo huku akisisitiza kuwa huo ni mkopo wa biashara na sio fedha za kula.

Baadhi ya wanufaika Masanja Mrisho na Sada Katamata, wamesema kuwa mikopo hiyo ni nguzo muhimu katika kukuza na kuendeleza biashara zao, huku akiahidi kuwa watazirejesha kwa wakati kama walivyoelekezwa. 
  
   

Comments

Popular posts from this blog

UONGOZI WA SHIRIKISHO LA VYAMA VYA TIBA ASILI TANZANIA WADAIWA SI HALALI NA UMEKOSA DIRA YA KUENDESHA VYAMA VYA WAGANGA WA TIBA ASILI

NAIBU WAZIRI NDERIANANGA AONGOZA UJUMBE WA TANZANIA KATIKA MKUTANO WA TATU WA KIMATAIFA WA WATU WENYE ULEMAVU UJERUMANI.