WAZEE TABORA WANENA MAZITO KWA RAIS SAMIA
Na Allan Kitwe,DmNewsonline
TABORA
ZIKIWA zimebakia siku chache kumalizika mwaka 2025 na kuanza mwaka mpya wa 2026, wazee wa Mkoa wa Tabora wameeleza kuridhishwa na utendaji wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan katika awamu yake ya pili baada ya kuingia madarakani.
Wameeleza kuwa weledi na ufanisi wa Kiongozi mzuri unapimwa kwa mambo makubwa matatu ambayo ni hali ya usalama wa nchi, kasi ya maendeleo na uchumi, mambo haya yamesimamiwa vizuri na nchi inapiga hatua kubwa.
Mzee Elisha Daud Mponeja ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi wa Jadi katika halmashauri ya manispaa Tabora ameeleza kuwa Rais Samia amefanya kazi nzuri sana katika kipindi chake cha miaka minne na hata sasa anaendelea vizuri.
Amefafanua kuwa baada ya kukabidhiwa nchi Machi 19, 2021 kutoka kwa mtangulizi wake aliyetangulia mbele za haki, Dkt John Pombe Magufuli, watanzania walishuhudia kasi kubwa ya utekekezaji miradi ya maendeleo katika sekta zote.
‘Katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wake mambo makubwa yamefanyika ikiwemo kuimarisha mahusiano mazuri kitaifa na kimataifa na miradi mikubwa ya kimkakati iliendelea kutekelezwa kwa kasi kubwa pasipo kusimama,’ ameeleza.
Aidha baada ya kuchaguliwa tena katika uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29 mwaka huu ameahidi kuendeleza kasi ile ile ya utekelezaji miradi ya maendeleo ikiwemo kuboresha huduma za kijamii na kuimarisha ulinzi na usalama wa nchi.
Mzee Mponeja amebainisha kuwa zikiwa zimepita takribani siku 55 tangu aapishwe tena kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa awamu ya pili, amedhihirisha weledi wake katika kusimamia maendeleo na usalama wa nchi.
Aidha miradi yote iliyoanza kutekelezwa katika awamu yake ya kwanza imeendelea kutekelezwa kwa kasi kubwa na yale yote aliyoahidi wakati wa kampeni za uchaguzi yameendelea kuratibiwa tayari kwa ajili ya utekelezaji.
Mzee Adamu Malunkwi, mkazi wa Urambo ameeleza kuridhishwa na utulivu mkubwa wa Rais Samia katika kutekeleza miradi ya maendeleo na kushughulikia masuala mbalimbali ya kitaifa na kimataifa kwa manufaa ya watanzania.
Ameeleza kuwa vurugu za Oktoba 29 zilisababisha nchi kutikisika na hali ya amani ilianza kutoweka, lakini kwa ujasiri mkubwa Rais amewatuliza watanzania, ameimarisha ulinzi na usalama wa nchi na kutoa wosia wa amani, nchi sasa imetulia.
Mzee Msagata Fundikira (Chifu wa Unyanyembe) ameongeza kuwa Rais Samia ni Kiongozi makini, anayetambua wajibu wake kwa jamii, ameonesha uwezo mkubwa wa kutumikia wananchi na kuimarisha ulinzi na usalama wa nchi.
Amebainisha kuwa Rais ana dhamira njema ya kuifanyia mambo makubwa nchi hii, ila akadokeza kuwa baadhi ya wasaidizi wake wanamwangusha, hawatekelezi wajibu wao ipasavyo kwa wananchi hali inayosababisha malalamiko.
Chifu Fundikira amemwomba Rais Samia kufanyia kazi yale yote yanayolalamikiwa na wananchi ili kuleta utulivu miongoni mwa jamii na nchi yetu iendelee kupiga hatua kubwa zaidi kimaendeleo. 







Comments
Post a Comment