DKT. PIMA AAGIZA WAKUU WA SHULE KUSIMAMIA NIDHAMU

   Na Allan Kitwe, DmNewsonline

                    TABORA


  WALIMU Wakuu wa shule za msingi na sekondari katika Halmashauri ya Manispaa Tabora wameagizwa kusimamia ipasavyo nidhamu za walimu na wanafunzi katika shule zao ili kuinua juu taaluma.  

Agizo hilo limetolewa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa hiyo Dkt John Pima alipokuwa akifunga semina maalumu ya Maafisa Elimu, Walimu wa Nidhamu, Waratibu na Wakuu wa shule zote mjini hapa.

Amesema kuwa serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imefanya maboresho makubwa ya miundombinu katika shule zote za Manispaa hiyo hivyo kuboreshwa mazingira ya ufundishaji na kujifunza.

‘Mazingira bora yaliyopo katika shule zetu ni chachu muhimu ya kuwezesha watoto wetu kufanya vizuri zaidi katika mitihani yao ya kitaifa hivyo kuongeza ufaulu katika manispaa yetu, katika hili ni lazima tuimarishe nidhamu’, ameeleza.

Dkt.Pima ameahidi kutoa motisha nzuri kwa kila mwalimu ambaye somo lake litapata alama A za ufaulu kwa idadi yoyote ile ya A, aidha, Mwalimu Mkuu na shule itakayoongoza kwa ufaulu nao watapata zawadi.

Kuhusu miradi, Dkt.Pima amewataka kusimamia ipasavyo fedha zote zinazopelekwa katika shule zao ili zifanye kazi iliyokusudiwa na thamani ya fedha ionekane, kinyume na hapo hatua za kiutumishi zitachukuliwa kwa yeyote atakayekwamisha.

‘Tunatumia fedha nyingi sana kutekeleza miradi ya elimu katika shule zetu, miradi hii ni lazima itekelezwe kwa wakati na iwe na ubora unaotakiwa, katika hili hatutamfumbia macho Mkuu wa shule yeyote atakayezembea’, amesema.

Akisoma maazimio ya semina hiyo, Mwalimu Raphael Mageni, Mratibu Elimu Kata wa Kata ya Mwinyi amesema kuwa shule kwa kushirikiana na wazazi/walezi na wadau watahakikisha wanafunzi wote wanapata chakula cha mchana shuleni.

Pia wamekubaliana kutokomeza utoro wa wanafunzi katika shule zao na kuwa na mfumo wa mitihani ya pamoja kwa shule zote zilizopo katika halmashauri hiyo ili kuongeza weledi na ushindani katika ufundaji watoto.

Aidha amesema kuwa watasimamia ipasavyo miradi inayotekelezwa katika shule zao ikiwemo nidhamu na uadilifu wa walimu na wanafunzi na kuwapa watoto elimu ya kujitegemea.   

Comments

Popular posts from this blog

UONGOZI WA SHIRIKISHO LA VYAMA VYA TIBA ASILI TANZANIA WADAIWA SI HALALI NA UMEKOSA DIRA YA KUENDESHA VYAMA VYA WAGANGA WA TIBA ASILI

NAIBU WAZIRI NDERIANANGA AONGOZA UJUMBE WA TANZANIA KATIKA MKUTANO WA TATU WA KIMATAIFA WA WATU WENYE ULEMAVU UJERUMANI.