DIWANI AGUSWA NA KERO ZA WAJAWAZITO TABORA
Na Allan Kitwe,DmNewsonline
TABORA
DIWANI wa Kata ya Chemchem katika halmashauri ya manispaa Tabora kupitia CCM, Bandola Salum Milambo ameanza mikakati ya kutatua kero wanazopata akinamama wajawazito na wagonjwa wengine katika kata yake.
Akizungumza na wanahabari jana ameeleza kuwa baada ya kuapishwa sasa ana kazi moja tu ya kuhakikisha kero zote zinazowakabili wapiga kura wake zinashughulikiwa ipasavyo na mamlaka husika.
Amedokeza kuwa kwa kuanzia anaanza na kero ya wajawazito ambao wamekuwa wakilalamikia kutozwa gharama kubwa wanapoenda kuanza kliniki kwenye Kituo cha kutolea huduma za afya cha Town Kliniki, kilichoko hapa Chemchem.
‘Nimepanga kutembelea Kituo hiki (Zahanati ya Town Kliniki) ili kujionea hali ya utoaji huduma lakini pia kufuatilia malalamiko ambayo yametolewa na akinamama wajawazito ya kutozwa gharama kubwa ili wapate huduma za kliniki’, ameeleza.
Amesema kuwa utaratibu wa wananchi kuchangia huduma za afya unajulikana, lakini inapobainika kuwa wanatozwa gharama kubwa kinyume na utaratibu hatuwezi kukaa kimya, ni lazima kuwe na maelezo ya kutosheleza.
Mheshimiwa diwani ameeleza kuwa baadhi ya watumishi sio wastaarabu, wanatoa lugha zisizo na staha kwa wagonjwa na akinamama wajawazito, hawana lugha ya ukarimu, hata ikitokea mwananchi amezidiwa hawajali, wanachoangalia ni hela tu.
Amebainisha kuwa kwenye kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani mwaka huu, Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan aliahidi kushughulikia baadhi ya kero za wananchi, ikiwemo sekta ya afya.
‘Kama mwakilishi wa wananchi, ni wajibu wangu kuhakikisha kero zinazolalamikiwa na wananchi zinatatuliwa, na leo hii nafuatilia kero ya mafuriko ya Mto Kenge ambayo yameleta adha kubwa kwa wananchi, amedokeza. 





Comments
Post a Comment