ASKOFU MEIVUKIE ATAKA UPENDO, HAKI NA AMANI VIDUMISHWE

   Na Allan Kitwe, DmNewsonline

                   TABORA 

ASKOFU wa Kanisa la TAG Jimbo la Tabora Kati na Kiongozi wa Kanisa la Kitete Christian Centre (KCC) la Mjini Tabora Rev. Paul Meivukie ameomba upendo, haki na amani viendelee kudumishwa nchini ili jamii iishi kwa utulivu.

Ametoa rai hiyo leo kwenye ibada ya sikukuu ya krismas ambapo ameeleza kuwa krismasi ni tukio kubwa linalobeba ujumbe wa upendo, haki na amani kwa watu wote, hivyo mamlaka na jamii kwa ujumla hawana budi kuyadumisha.

Amesisitiza kuwa tunapoadhimisha sikukuu hii ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo hatuna budi kumwomba Mungu ili taifa liendelee kuwa na amani na utulivu na upendo na haki viendelee kudumishwa wakati wote ili Mungu aliinue taifa lake.

‘Taifa liliingia kwenye wakati mgumu sana Oktoba 29, 2025 siku ya uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani, hili halipaswi kufumbiwa macho, kama taifa tunapaswa kusameheana na kupendana ili kudumishwa amani yetu', amesema.

Askofu Meivukie ameasa waumini wa kanisa hilo na jamii kwa ujumla kuishi tabia na maisha ya Yesu Kristo na kuachana na njia zisizofaa ambazo hupelekea kujengeka chuki na hatimaye kusababisha uvunjifu wa amani.

Akinukuu maandiko kwenye kitabu cha Isaya 9:6 ameeleza kuwa mtoto Yesu alizaliwa kwa ajili yetu, ana uweza wa kifalme, ni mshauri wa ajabu, Mungu mwenye nguvu, Baba wa Milele na Mfalme wa amani.

Amesisitiza kuwa yeyote atakayemkubali Yesu kuwa Bwana na Mwokozi wa maisha yake hatapotea kamwe, atakuwa salama na maisha yake hayatakuwa kama yalivyokuwa huko nyuma, atakuinua kiroho, kimwili na kiuchumi pia.

‘Yesu akiingia ndani yako tabia yako inabadilika, milango ya baraka inafunguka, amani na upendo vinatawala na unakuwa salama, kupitia sikukuu hii kila mmoja atafakari njia zake na kubadilika ili Kristo afanye makao ndani yake’, ameeleza.  

Askofu Meivukie amesisitiza kuwa Yesu Kristo ni zawadi ya Mwenyezi Mungu kwa watu wote hapa duniani kama ilivyoandikwa katika kitabu cha Luka Mtakatifu 2: 10-11 …..maana katika Mji wa Daudi amezaliwa Mwokozi, ndiye Kristo Bwana.   



Comments

Popular posts from this blog

UONGOZI WA SHIRIKISHO LA VYAMA VYA TIBA ASILI TANZANIA WADAIWA SI HALALI NA UMEKOSA DIRA YA KUENDESHA VYAMA VYA WAGANGA WA TIBA ASILI

NAIBU WAZIRI NDERIANANGA AONGOZA UJUMBE WA TANZANIA KATIKA MKUTANO WA TATU WA KIMATAIFA WA WATU WENYE ULEMAVU UJERUMANI.