NIDA, WANANCHI NENDENI MKACHUKUWE VITAMBULISHO ILI MUENDELEE KUPATA HUDUMA.

 Na Timoth Marko,DmNewsonline

            DAR ES SALAAM

MKURUGENZI wa  Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), James Kaji amesema Mamlaka hiyo imetoa kibali maalum cha muda wa mwaka mmoja kwa ajili ya kushughulikia maombi ya marekebisho ya taarifa za wananchi kwenye Mfumo wa Utambulisho wa Taifa, kuanzia Oktoba 2025.

Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es salaam na mkurugenzi huyo katika mkutano wake na waandishi wa habari ambapo amesema kibali hicho kimetolewa ili kuwasaidia wananchi waliokumbwa na changamoto mbalimbali za usajili, ambazo awali zilishindikana kufanyiwa marekebisho kutokana na ukinzani wa miongozo iliyokuwepo.

Amesema kibali hicho kinahusu makundi manne maalumu ambayo ni waathirika wa vyeti vya kughushi, wakiwemo waliowahi kufutwa kazi Serikalini na ambao taarifa zao za usajili wa NIDA zinatokana na vyeti hivyo pamoja na Watu waliotumia majina ya watu wengine kupata vyeti vya elimu. 

Amesema kundi lingine ni wale  waliotoa taarifa za uongo wakati wa usajili wa NIDA pamoja na  Raia wa Tanzania waliojisajili kama wakimbizi.

"Wananchi wa makundi haya wanatakiwa kufika katika ofisi za NIDA za wilaya wakiwa na nyaraka muhimu kama vile vyeti halisi vya elimu, cheti cha kuzaliwa kilichohakikiwa na RITA, deed poll iliyosajiliwa na kuchapishwa katika gazeti la Serikali, pamoja na nyaraka nyingine zitakazohitajika kulingana na aina ya marekebisho."alisema Kaji

Pia amesisitiza kuwa maombi yatakayokidhi vigezo pekee ndiyo yatashughulikiwa, na kutoa tahadhari kuwa kutoa taarifa za uongo ni kosa la kisheria chini ya Sheria ya Usajili na Utambuzi wa Watu.

Mkurungezi huyo Mtendaji amewataka wananchi kutumia fursa hii mapema kwa kuwa kibali hiki ni cha muda maalum wa mwaka mmoja pekee.

"Nawaomba wananchi  wote wanaohusika kujitokeza mapema ili kuhakikisha taarifa zao kwenye mfumo wa Taifa zinarekebishwa kwa mujibu wa sheria na taratibu"alisema Kaji 

Aidha amewahakikishia wananchi  hakuna mtu yoyote atakayechukuliwa hatua za kushitakiwa au kutozwa  gharama zozote hivyo wajitokeze 

Katika hatua nyingine amewaomba wananchi wale ambao bado awajachukua Vitambulisho vya Taifa  kwenda kuvichukua ili waendelee kupata huduma mbalimbali.

Comments

Popular posts from this blog

UONGOZI WA SHIRIKISHO LA VYAMA VYA TIBA ASILI TANZANIA WADAIWA SI HALALI NA UMEKOSA DIRA YA KUENDESHA VYAMA VYA WAGANGA WA TIBA ASILI

NAIBU WAZIRI NDERIANANGA AONGOZA UJUMBE WA TANZANIA KATIKA MKUTANO WA TATU WA KIMATAIFA WA WATU WENYE ULEMAVU UJERUMANI.