ASAS : WANANCHI JITOKEZENI KUPIGA KURA MSIWE NA HOFU .
Na Eliasa Ally,DmNewsonline
IRINGA
MJUMBE wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Salim Abri Asas amewataka wananchi katika Halmashauri ya Mji Mafinga kujitokeza kwa wingi kupiga kura kwenye Uchaguzi Mkuu na kuwaondoa hofu ya kuwa siku hiyo kunaweza kuwa na vitendo vya vurugu kama ambavyo imekuwa ikienezwa kwenye mitandao ya kijamii na baadhi ya watu wenye nia ovu.
Katika siku za hivi karibuni kumezuka wimbi la baadhi ya watu kutoka ndani na nje ya nchi ambao kwa nyakati tofauti wamekuwa wakiyashawishi makundi mbalimbali katika jamii likiwemo kundi la vijana kufanya maandamano na kuchochea ghasia ambazo zitaathiri zoezi hilo la Uchaguzi na amani kwa ujumla wapuuzwe.
Asas ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa amesema hayo wakati akihutubia maelfu ya wana CCM na wananchi kwa ujumla waliofurika kwenye Mkutano Mkubwa wa Kufunga Kampeni za Chama hicho kwa Jimbo la Mafinga Mjini uliofanyika katika kijiji cha Ugute kata ya Isalavanu katika Mjini Mafinga.
"Natarajia Oktoba29 mwaka huu mtakutokeza kwa wingi kupiga kura Msiogope wala kuwa na hofu, amani ipo, kutakuwa na ulinzi wa kutosha. Nchi yetu imetulia hayo yote ni maneno ya mitaani"- Amesema Asas.
Amesema nchi imetulia na ipo kwenye mikono salama ya vyombo vya Ulinzi na Usalama hivyo wananchi wanapaswa kutumia hali hiyo kama kichocheo cha kwenda kushiriki Uchaguzi Mkuu na kutimiza haki yao ya Kikatiba ya kupiga kura .
Kwa upande wake, Mgombea Ubunge Jimbo la Mafinga Mjini, Dickson Lutevele maarufu kama 'Villa' amesema ana imani kubwa na wananchi kwenda kwenye vituo vya kupigia kura kwa wingi kama sehemu ya kuonyesha shukrani kwa Serikali kutokana na mambo makubwa iliyoyafanya hasa katika eneo la miradi ya maendeleo.
Aidha, Mgombea huyo amewasisitizia wananchi bila ya kujali itikadi za kisiasa au imani zao za kidini kuona umuhimu wa kutanguliza amani ambayo ndio msingi wa maendeleo jumuishi na endelevu.
"Ni imani yangu Mufindi kwa mara nyingine tena tutaongoza kwa wingi wa kura kukichagua Chama Cha Mapinduzi kama kawaida yetu"- Amesema Villa.

Comments
Post a Comment