WAKAZI UKUMBISIGANGA WAFURAHIA UJENZI KITUO CHA AFYA

Na Allan Kitwe, Tabora

WAKAZI wa Kata ya Ukumbisiganga Wilayani Kaliua wameeleza kufurahishwa na hatua ya serikali ya awamu ya sita kupeleka zaidi ya shilingi milioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha afya ili kuboresha huduma za afya.

Wakizungumza na gazeti hili baadhi ya wananchi wameeleza kuwa Kata yao ni miongoni mwa kata zilizokuwa na changamoto kubwa ya upatikanaji huduma za afya, lakini serikali imesikia kilio chao na kuanza ujenzi wa kituo hicho.

Mohamed Ramadhan (57) mkazi wa Kijiji cha Usinga katika kata hiyo, ameishukuru serikali inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwajengea kituo hicho ambacho kitasaidia kuokoa maisha ya akinamama, wajawazito, wazee na watoto.

Ameeleza kuwa wakazi wa kata hiyo yenye vijiji vinne vya Ukumbi-Siganga, Lumbe, Usinga na Ukumbi-Kakoko wamekuwa wakipata huduma za afya kwenye zahanati lakini wanapohitaji huduma za matibabu makubwa hawazipati.

‘Vijiji vyetu vipo umbali wa zaidi ya km 90 kutoka Makao Makuu ya Wilaya, hali inayopelekea upatikanaji huduma za kijamii kuwa shida kubwa, mama yetu Rais Samia amesikia kilio chetu, sasa ameanza kutujengea kituo cha afya’, amesema.

Mkazi wa Lumbe, Lucia Mndala (50) ameeleza kuwa akinamama wa Vijiji hivyo sasa wana amani kwa kuwa muda si mrefu wataanza kupata huduma za uhakika ikiwemo upasuaji, picha za mionzi (x-ray) na uchunguzi wa afya zao.

‘Akinamama wa kata hii tumejawa na furaha kubwa na mwaka huu tunajambo letu kwa mama, Oktoba 29 tunaahidi kumpa kura za kumwaga ili andelee kutuletea maendeleo, na kushughulikia kero zetu nyingine’, ameeleza.

Amebainisha changamoto nyingine zilizopo kuwa ni ukosefu wa barabara ya uhakika inayounganisha makao makuu ya kata hiyo na vijiji, maji na umeme, mambo ambayo alisema kuwa ni madogo sana kwa Rais Samia.

Akiongea katika mkutano wa kampeni uliofanyika jana katika vijiji vya Ukumbi-Kakoko na Usinga, mgombea ubunge wa Jimbo la Kaliua kupitia CCM Joseph Enock ameahidi kusimamia ipasavyo utatuzi wa changamoto hizo.

Ameeleza kuwa ilani ya uchaguzi ya CCM ya 2025-2030 imeeleza bayana kuwa ardhi yote ya Wilaya hiyo itapimwa ili kumaliza migogoro iliyopo, hivyo akawahakikishia kuwa serikali itapima maeneo yao na kumaliza mgogoro uliopo.

Amedokeza kuwa Rais Dk Samia ni kiongozi makini na msikivu, hivyo ana uhakika vijiji 2 vya kata hiyo ambavyo bado vipo kwenye hifadhi atalishughulikia ili wananchi waishi kwa amani na utulivu hivyo akaomba Oktoba 29 wawape kura za kishindo mgombea Urais, ubunge na udiwani kupitia CCM.     

Comments

Popular posts from this blog

UONGOZI WA SHIRIKISHO LA VYAMA VYA TIBA ASILI TANZANIA WADAIWA SI HALALI NA UMEKOSA DIRA YA KUENDESHA VYAMA VYA WAGANGA WA TIBA ASILI

NAIBU WAZIRI NDERIANANGA AONGOZA UJUMBE WA TANZANIA KATIKA MKUTANO WA TATU WA KIMATAIFA WA WATU WENYE ULEMAVU UJERUMANI.