TASAC Yawataka Wachimbaji Kutotumia Kampuni Binafsi Kusafirisha Kemikali na Vilipuzi
Richard Mrusha,DmNewsOnline
GEITA
Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limepiga marufuku kwa kampuni binafsi kujihusisha na usafirishaji wa kemikali na vilipuzi vinavyotumika katika shughuli za uchimbaji migodini, likisisitiza kuwa jukumu hilo ni la TASAC pekee.
Mkurugenzi wa Huduma za Shirika hilo, Hamid Mbegu ameyasema hayo katika Maonesho ya Nane ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yaliyofanyika mkoani Geita.
Amesema kwa mujibu wa Sheria ya Uwakala wa Meli, Sura ya 415, TASAC imepewa mamlaka ya kusimamia kwa ukamilifu usafirishaji na uondoshaji wa shehena zote hatarishi zikiwemo baruti na kemikali.
"Baadhi ya shehena hizi ni sumu na zina madhara makubwa."
Serikali kupitia TASAC ndiyo yenye mamlaka ya kusimamia hatua zote za uondoshaji wake. Makampuni yanayopitisha kemikali hizi kupitia kampuni binafsi yanakiuka sheria," alisisitiza Mbegu.
Ameongeza kuwa baadhi ya makampuni yamekuwa yakisafirisha kemikali hatarishi kama Sodium Cyanide kupitia njia zisizo rasmi, jambo linalohatarisha usalama wa watu na mazingira.
TASAC imewataka wachimbaji wadogo na wakubwa, pamoja na kampuni za uagizaji na usafirishaji, kufuata sheria na kuhakikisha shughuli zote za usafirishaji wa kemikali hizo zinafanywa kwa usimamizi wa wataalam wake pekee.




Comments
Post a Comment