MWINGIRA : TBA KUENDELEA KUTEKELEZA MIRADI MIKUBWA YA MAENDELEO
Na Richard Mrusha,DmNewsOnline
GEITA
Afisa Habari wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Adam Mwingira, amesema TBA inaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo ikiwa ni sehemu ya maboresho katika sekta ya ujenzi wa miundombinu ya umma. Ameyasema hayo leo wakati akizungumza katika Banda la TBA kwenye Maonesho ya Madini ya Geita, alipokuwa akipokea ugeni wa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko.
Akielezea mafanikio na mwelekeo wa taasisi hiyo, Mwingira amesema TBA ina mradi mkubwa unaotarajiwa kuanza kutekelezwa hivi karibuni, na kushukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuruhusu mazingira bora ya utekelezaji wa miradi hiyo kupitia mabadiliko ya sheria ya Majengo, GN Na. 595 ya mwaka 2023.
"Marekebisho haya yameruhusu TBA kushirikiana na sekta binafsi pamoja na taasisi za kifedha, jambo ambalo litaongeza kasi ya utekelezaji wa miradi kwa ubora na kwa wakati," amesema Mwingira.
Aidha, amewakaribisha wawekezaji wote wenye nia ya kushirikiana na TBA kwa njia ya ubia katika miradi ya ujenzi, akisisitiza kuwa taasisi hiyo iko wazi kwa ushirikiano wa aina hiyo ili kuhakikisha maendeleo yanawafikia wananchi kwa haraka.
Akitaja baadhi ya miradi mikubwa inayotekelezwa na TBA, Mwingira amesema ni pamoja na ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Chato na Hospitali ya Mkoa wa Geita, ambazo zimekuwa chachu ya maboresho ya huduma za afya kwa wananchi wa maeneo hayo.
Miradi mingine aliyotaja ni pamoja na kukamilika kwa ujenzi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita, pamoja na miradi inayoendelea kama vile ujenzi wa ofisi za TANESCO na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya.


Comments
Post a Comment