Mkurugenzi STAMICO Afanya Mazungumzo na Wanawake Wachimbaji wa TAWOMA
Na Richard Mrusha,DmNewsOnline
Geita
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Bw. CPA Venance Mwase amekutana na kufanya mazungumzo na wanachama wa Chama cha Wanawake Wachimbaji Madini Tanzania (TAWOMA) katika Maonesho ya Nane ya Teknolojia na Uwekezaji kwenye Sekta ya Madini yanayoendelea mkoani Geita.
Katika mazungumzo hayo, CPA Venance Mwase aliwapongeza wanawake hao kwa kazi nzuri wanayoifanya katika sekta ya madini huku akisisitiza dhamira ya STAMICO kuendelea kuwaunga mkono kwa vitendo.
“Kushukuru ni jambo jema, lakini niwaambie kuwa mnafanya kazi nzuri sana. Ukiona Salma anakuja kwangu na anatoka na kitu, jua nahamasishwa na mnachokifanya. Ahadi yangu kwenu ni kuendelea kuwashika mkono kwa sababu hamjawahi kuniangusha,” alisema CPA Mwase
Aliongeza kuwa serikali kupitia STAMICO itaendelea kuwapa fursa zaidi wanawake wachimbaji, hasa wale wanaojitokeza na kuonyesha juhudi. Alitaja kuwa STAMICO imejipanga kuwasaidia zaidi, ikiwa ni pamoja na kutoa vifaa muhimu kama pampu za maji.
“Nimeahidi mwenyewe kuhusu pampu za maji, kamilisheni utafiti wenu na mtuletee mahitaji. Tutaanza kutoa vifaa hivyo kwa awamu hadi kila mwanamke aondokane na changamoto ya upatikanaji wa maji kwenye maeneo ya uchimbaji,” aliongeza.
Katika mazungumzo hayo, Mkurugenzi huyo pia alieleza kuwa serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imekuwa na dhamira ya dhati ya kuwawezesha wachimbaji wadogo, hususan wanawake na vijana. Alibainisha kuwa moja ya rigs za kisasa iliyoletwa nchini kwa maelekezo ya Rais, imeelekezwa kwa wanawake wachimbaji, na STAMICO iko mbioni kukamilisha vifaa na taratibu za makabidhiano.
Kwa upande wake, Katibu wa TAWOMA Taifa Salma Ernest alishukuru STAMICO kwa kuwa bega kwa bega na wanawake katika shughuli zao za uchimbaji, huku akieleza kuwa Geita ndio mkoa uliyonufaika zaidi kupitia mradi wa Malika wa Madini unaosimamiwa na STAMICO.
“Mapendekezo yetu ya kuhamasisha vikundi vingi kujiunga na TAWOMA yameanza kutekelezwa kwa mafanikio makubwa. Pia tulipendekeza STAMICO itoe elimu na vifaa, na tumeshuhudia zaidi ya wanawake 640 wakinufaika na elimu hiyo. Pia kati ya jokarasha 20 zilizopo nchini, tano zipo Geita,” alisema Katibu huyo.
Aidha, wanawake hao walieleza kufurahishwa na ushiriki wao kwenye maonesho ya mwaka huu, wakisema kuwa yamewapa fursa ya kutambulika, kujifunza teknolojia mpya na kuunganishwa na taasisi za kifedha pamoja na wawekezaji.
Mwenyekiti wa TAWOMA mkoa wa Geita Evelyne Cleophace naye alitoa shukrani kwa Mkurugenzi Mrusha, akimtaja kuwa "baba bora" kwa wanawake hao kutokana na namna anavyowasikiliza na kuwatafutia suluhisho la changamoto zao.








Comments
Post a Comment