MHIFADHI MDOE ATOA ELIMU KUHUSU UHIFADHI WA MAZINGIRA KATIKA MAONESHO YA MADINI GEITA




Na Richard Mrusha,DmNewsOnline
GEITA

Mhifadhi Mwandamizi kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Juma Mdoe amesema kuwa wachimbaji wa madini ni miongoni mwa wadau wakuu wa rasilimali za misitu kutokana na shughuli zao kuhusisha matumizi makubwa ya miti, hivyo wana wajibu wa kushiriki katika juhudi za uhifadhi wa mazingira kwa kurudisha uoto wa miti wanaoiharibu.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Maonesho ya Nane ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika mkoani Geita, Mdoe alisema kuwa wameamua kushiriki kwenye maonesho hayo ili kutoa elimu kwa wadau mbalimbali, hususan wachimbaji, kuhusu umuhimu wa kuhifadhi mazingira.

Alisema kuwa wachimbaji wengi hutumia miti kutengeneza maboksi ya kuzuia udongo kusitiririka kwenye migodi, na hivyo wanapaswa kutambua kuwa wanalo deni la kuhakikisha uoto wa asili wa miti unarejeshwa.
 “Wanapaswa kutambua kuwa wana wajibu wa kurudisha uoto wa miti na kuendelea na juhudi za uhifadhi kwa kupanda miti kwa wingi. Wao ni watumiaji wakubwa wa miti, hivyo ni lazima washiriki katika kuurejesha uoto huo,” alisema Mdoe.

Aliongeza kuwa katika maonesho hayo, Taasisi ya Huduma za Misitu Tanzania (TFS) inatoa elimu kwa jamii kuhusu shughuli mbalimbali za uhifadhi na umuhimu wake, ikiwa ni pamoja na faida za misitu kwa upande wa ikolojia, utoaji wa hewa safi, upatikanaji wa samani, vyanzo vya maji, na matumizi ya misitu katika ufugaji wa nyuki.

Mdoe pia alisema kuwa misitu inatoa faida nyingi za kiafya na kiuchumi, na kwamba elimu hiyo inalenga kuwahamasisha wananchi kujiepusha na ukataji hovyo wa miti pamoja na kuhamasisha utalii wa mazingira, hususan utalii wa ikolojia.

Alitaja baadhi ya maeneo ya hifadhi zinazotunzwa na TFS kuwa ni pamoja na hifadhi ya mazingira asilia ya Kome iliyopo Sengerema, shamba la miti la Silayo lenye fursa mbalimbali ikiwemo utalii wa nyuki na uoto wa asili, pamoja na shamba la miti la Rubare lililopo Kagera ambalo ndani yake kuna maporomoko ya maji.

Aidha, alizitaja hifadhi nyingine za mazingira asilia kuwa ni pamoja na Amani, Magamba, Minziro, na maeneo ya utalii wa picha na wanyama adimu wanaopatikana ndani ya hifadhi hizo hapa nchini.

Akiihamasisha jamii inayoishi pembezoni mwa hifadhi, Mdoe alisema TFS inatoa huduma ya kuruhusu wadau wa ufugaji wa nyuki kutumia maeneo ya hifadhi au mashamba yao kwa kuingiza mizinga, ili kufanya shughuli hizo kwa mujibu wa utaratibu rasmi na kwa kuzingatia kanuni za uhifadhi.

 “Tunatoa vibali rasmi 
kwa ajili ya shughuli za ufugaji wa nyuki ndani ya hifadhi. Hii ni kwa sababu maeneo haya yanalindwa vizuri, na hivyo ni salama kwa uzalishaji wa asali na bidhaa nyingine za nyuki,” alieleza.




Comments

Popular posts from this blog

UONGOZI WA SHIRIKISHO LA VYAMA VYA TIBA ASILI TANZANIA WADAIWA SI HALALI NA UMEKOSA DIRA YA KUENDESHA VYAMA VYA WAGANGA WA TIBA ASILI

NAIBU WAZIRI NDERIANANGA AONGOZA UJUMBE WA TANZANIA KATIKA MKUTANO WA TATU WA KIMATAIFA WA WATU WENYE ULEMAVU UJERUMANI.