Aweso Apongeza Usimamizi Mradi wa Maji Chato Uliofikia 53%, Wananchi Waomba Uharakishwaji
Na Mwandishi wetu,DmNewsonline
GEITA
WAZIRI wa Maji, Jumaa Aweso, amewapongeza wasimamizi wa mradi wa maji wa miji 28 unaoendelea kutekelezwa wilayani Chato kwa usimamizi mzuri, huku akieleza kuridhishwa na maendeleo ya utekelezaji ambao kwa sasa umefikia asilimia 53.
Akizungumza wakati wa ziara yake ya kukagua mradi huo, Waziri Aweso alisema hatua iliyofikiwa ni ya kutia moyo na kuonyesha dhamira ya dhati ya serikali ya kuwapatia wananchi huduma bora ya maji safi na salama.
Katika ziara hiyo, wananchi wa Kijiji cha Mkungo, Kata ya Mkome, waliiomba serikali kupitia Wizara ya Maji kuharakisha utekelezaji wa mradi huo ili kuondokana na adha ya upatikanaji wa maji safi inayowakumba kwa muda mrefu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Wilaya ya Chato (CHAWASA), Aisaki Mgeni, alieleza kuwa mradi huo unatarajiwa kugharimu jumla ya shilingi bilioni 41 hadi kukamilika, na utaongeza uzalishaji wa maji kutoka lita milioni 4 hadi milioni 10 kwa siku, ikiwa ni zaidi ya mahitaji ya sasa ya lita milioni 8 kwa siku.
“Mradi huu utakapokamilika utahudumia zaidi ya wananchi laki moja wa Wilaya ya Chato na kumaliza kabisa changamoto ya upatikanaji wa maji safi,” alisema Mgeni.
Waziri Aweso alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi ya maji nchini ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma stahiki kama ilivyo dhamira ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kumtua mama ndoo kichwani. 













Comments
Post a Comment