ABSA DAR CITY MARATHON YAKABIDHI VIFAA TIBA KWA WANAWAKE WAJAWAZITO NA WATOTO HOSPITALI YA MNAZI MMOJA
Na Mwandishi wetu,DmNewsOnline
Dar Es Salaam.
Katika kuimarisha Huduma za Afya ya Uzazi nchini
Klabu ya Riadha ya 'The Runners, imetoa vifaa tiba kwa wanawake wajawazito na watoto wachanga katika Hospitali ya Mnazi mmoja jijini Dar es salaam.
Vifaa hivyo ni kipimajoto cha kidigitali, seti za sindano maalum (cannulas), na kifaa cha kufuatilia afya ya mtoto tumboni (fetal monitor)
Akizungumza na Waandishi wa habari wakati wa hafla ya makabidhiano, msemaji wa klabu hiyo, Godphrey Mindu, amesema kuwa vifaa hivyo ni kwa ajili ya watoto walioko tumboni,waliotoka kuzaliwa pamoja na wanawake wajawazito.
Ameongeza kuwa vifaa hivyo vimetolewa kama sehemu ya kuiunga mkono serikali na Rais Samia Suluhu Hassan katika juhudi zake za kuboresha huduma ya mama na mtoto na kuhakikisha usalama wa mama wajawazito na watoto wao
Ametoa wito kwa wadau wengine kuungana na serikali kuboresha huduma ya afya kwa ajili ya kuokoa maisha ya wengine.
Kwa upande wake, Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Dk Linda Mutasa, alieleza kuwa msaada huo umekuja wakati muafaka kwa sababu kulikuwa na upungufu wa vifaa hivyo vya huduma ya dharura kwa wanawake wajawazito na watoto.
“Vifaa hivi vitatusaidia kuboresha ufuatiliaji wa afya ya mama na mtoto kuanzia akiwa tumboni, wakati wa kuzaliwa na baada ya kuzaliwa na kusaidia kuokoa maisha yao kwa hiyo tunashukuru sana kwa msaada huu,” alisema Dk Mutasa.
Comments
Post a Comment