ULENGE ATOA VIFAA VYA UJENZI NYUMBA ZA MAKATIBU UWT KOROGWE

Na Yusuph Mussa,DmNewsonline

            Korogwe

MBUNGE  wa Viti Maalumu Mkoa wa Tanga Mhandisi Mwanaisha Ulenge ametoa msaada wa vifaa vyenye thamani ya sh. milioni 5,320,000 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa nyumba ya Katibu wa UWT Wilaya ya Korogwe Vijijini na Katibu wa UWT Wilaya ya Korogwe Mjini. 

Kwa nyumba ya Katibu wa UWT Korogwe  Vijijini ametoa mifuko 100 ya Saruji yenye thamani ya sh. milioni 1.7. nondo 35 zenye thamani ya sh. 770,000  tripu tatu  za mchanga zenye thamani ya sh. 270,000, na usafiri wa saruji hadi eneo la mradi (Site) sh. 480,000, hivyo jumla kuwa sh 3,120,000. Wakati kwa nyumba ya Korogwe Mjini ametoa mifuko 100 ya Saruji ya sh. milioni 1.7 na nondo 25 zenye thamani ya sh. 500,000 jumla kuwa sh. milioni 2.2.

Ametoa vifaa hivyo alipotembelea na kuona ujenzi wa nyumba ya Katibu huyo inayojengwa kwenye Makao Makuu mapya ya Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe, Kijiji cha Makuyuni, ambapo alikuta wameanza ujenzi kwa kuchimba msingi.

Katibu wa Ujenzi nyumba ya Katibu wa UWT Wilaya ya Korogwe Vijijini Neema Barani alisema wameanza kuchimba msingi, lakini kama watapata mifuko 100 ya saruji na nondo 70 na tripu 10 za mchanga, wana uwezo wa kujenga hadi usawa wa boma (linta), na baadae kumalizia nyumba hiyo yenye vyumba vitatu, sebule na jiko.

Kutokana na mahitaji hayo, ndipo Mhandisi Ulenge akasema amewaletea mifuko ya saruji 100, lakini ataweza kuchangia nondo 35 na mchanga tripu tatu ili waweze kuanza ujenzi wa nyumba hiyo.

Akizungumza na Wajumbe wa Baraza la UWT Wilaya ya Korogwe Mjini kwenye kikao kilichofanyika Ukumbi wa CCM, Mhandisi Ulenge aliwataka wanawake kuwa na shughuli za kiuchumi ikiwa ni pamoja na kilimo, ufugaji na ujasiriamali, kwani anataka wanawake wanapoazimisha Siku ya Mwanamke Duniani, kila mmoja aoneshe ameshika nini mkononi. 

Mhandisi Ulenge amejipambanua kuwa kazi aliyopewa na wanawake wa Mkoa wa Tanga ameifanya kwa kadri Mungu alivyomjalia, kwani ameweza kuwawezesha wanawake mbegu za mazao mbalimbali ili waweze kupanda na kuweza kujikwamua kiuchumi, ambapo kupitia Katibu  wa UWT Wilaya ya Korogwe Mjini Suzan Mandia, amesema wameshukuru kwa kupata mbegu hizo, na wanawake walifanyia kazi wao na familia zao, na kuweza kupata mavuno.

Mhandisi Ulenge amewaasa wajumbe hao kuwa mwaka huu ni wa Uchaguzi Mkuu, hivyo wanapokwenda kuchagua waweze kuchagua viongozi wenye dhamira ya dhati ya kuweza kuwasaidia wanawake hao. Na yeye kama Mbunge wa Mkoa wa Tanga, ameonesha dhamira hiyo kwa  vitendo kwa kuhakikisha wanawake wa mkoa huo wanapambana kuona hali zao za maisha zinakuwa bora kwa wao kujitafutia kipato chao.

"Chagua kiongozi kwa ajili ya maendeleo yako. Unapokuwa unakwenda kuchagua ni lazima uchague kile ambacho unaamini kitakuletea matokeo chanya kwenye jamii yako. Samia Suluhu Hassan na Chama Cha Mapinduzi kiliweka Ilani mbele, na ikaweza kujinadi kwa ilani. Na inapofika hii 2025, chama chetu kinaeleza kimefanya nini ndani ya miaka mitano ili wananchi waweze kukiamini tena. Na sisi tunatembea na kujigamba kwa kueleza yaliyofanywa na chama chetu 

"Na nataka kuwausia, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametekeleza Ilani yetu kwa kishindo, na ndiyo maana tunasema Samia mitano tena. Kigezo hicho hicho ndiyo cha kuangalia kwa viongozi wengine wabunge na madiwani kwa mambo waliyoyafanya kipindi cha miaka mitano. Kila mtu amefanya kwa ngazi yake, na kila mtu amefanya Mungu alivyomuwezesha, lakini ni sumu, tena simu kwa maendeleo yetu tusipomchagua mtu kwa kuangalia namna mtu alivyowajibika" amesema Mhandisi Ulenge. 


Comments

Popular posts from this blog

KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE TAMISEMI YAKOSHWA NA UBORA WA MIRADI YA MAENDELEO KIBAHA TC

MAMBO 10 MAZITO YANAYOIANGAMIZA NA KUIZAMISHA CHADEMA 2024/2025