TABORA YAONGOZA KIWANGO CHA MAAMBUKIZI YA MALARIA KWA ASILIMIA 23.
Na Deborah Lemmubi,DmNewsonline
DODOMA
WAZIRI wa Afya Mhe Jenista Mhagama amesema kuwa Takwimu zinaonesha kuwa Mkoa wa Tabora unaongoza kwa kuwa na kiwango kikubwa cha maambukizi ya Malaria kwa asilimia 23,huku Takwimu zikionesha kiwango cha Nchi kupungua kwa asilimia 45 kutoka asilimia 14.8 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 8.1 mwaka 2022.
Waziri Mhagama amesema hayo Jijini Dodoma Aprili 25,2025 wakati akizungumza na Waandishi wa Habari akitoa Taarifa ya Maambukizi hayo Kitaifa katika siku ya Maadhimisho ya Malaria Duniani inayoongozwa na kauli mbiu inayosema "Malaria Inatikomezwa na sisi: Wekeza Chukua Hatua -Ziro Malaria Inaanza na Mimi".
Na kusema kuwa pamoja na kuwepo kwa Mikoa yenye maambukizi ya juu lakini pia ipo Mikoa yenye kiwango cha chini cha Maambukizi ya Malaria ya chini ya asilimia moja ikiwemo Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Dodoma, Songwe, Mwanza, Dar Es Salaam,Iringa na Singida.
"Takwimu hapa nchini kwetu zinaonesha kiwango cha maambukizi ya ugonjwa wa Malaria kimepungua kwa takribani asilimia 45 kutoka asilimia 14.8 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 8.1 mwaka 2022".
"Takwimu hizo zinaonesha Mkoa wa Tabora unaongoza kuwa na kiwango kikubwa cha maambukizi ya Malaria kwa asilimia 23, ukifuatiwa na Mkoa wa Mtwara wenye kiwango cha maambukizi asilimia 20, Kagera asilimia 18, Shinyanga asilimia 16 na Mkoa wa Mara wenye asilimia 15. Aidha, mikoa yenye kiwango cha chini cha maambukizi ya malaria kwa chini ya asilimia moja ni Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Dodoma, Songwe, Mwanza, Dar Es Salaam, Iringa, na Singida".
Pia ametumia nafasi hii kutoa ujumbe kwa Watanzania wote katika siku hii ya Malaria Duniani kuendelea kuchukua hatua stahiki katika mapambano dhidi ya Malaria kwa kushiriki katika kudhibiti Mazalia ya mbu kwenye mazingira yanayowazunguka kwa kufukia madimbwi yanayoruhusu maji kutuama kwa muda mrefu ili kuzuia mbu kuzaliana.
"Nitoe wito kwa jamii yote ya Tanzania juu ya kuendelea kuchukua hatua stahiki katika mapambano dhidi ya ugonjwa malaria kwa:Kushiriki katika kudhibiti mazalia ya mbu kwenye mazingira yanayowazunguka kwa kufukia madimbwi yanayoruhusu maji kutuama kwa muda mrefu ili kuzuia mbu kuzaliana na kutoa ushirikiano katika unyunyiziaji wa viuadudu vya kibaiolojia".
"Kulala kwenye chandarua chenye dawa kila siku, kushona vyandarua vyetu pale vinapochanika ili kuviwezesha kudumu kwa muda unaotarajiwa wa miaka ,Kuwahi katika Vituo vya huduma za afya mara tunapohisi dalili za malaria ili tupime kuthibitisha uwepo wa vimelea vya malaria kabla ya kutumia dawa kwani sio kila homa ni malariaKutumia dawa Mseto kutibu malaria na kuhakikisha tunamaliza dozi kulingana na maelekezo ya watoa huduma ili kuweza kupona na kuzuia usugu wa vimelea vya malaria dhidi ya dawa".
Siku ya Malaria Duniani, huadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 25 Aprili ambapo katika siku hii, Tanzania inaungana na nchi nyingine duniani kuadhimisha kumbukumbu ya mapambano dhidi ya ugonjwa wa malaria. Aidha, siku hii inalenga katika kutathmini utekelezaji wa mikakati na afua za za kudhibiti ugonjwa wa malaria, mafanikio yaliyopatikana kutokana na jitihada za Serikali na wadau. 

Comments
Post a Comment