KOROGWE TC WAENDELEA KUTOA ELIMU MALIPO YA TASAF

Na Yusuph Mussa,DmNewsonline

            Korogwe

MFUKO wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) Halmashauri ya Mji Korogwe mkoani Tanga umeendelea kupata mafanikio kwa kuweza kuwaelimisha wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya za Walengwa kuwa wanahakikisha wanaendelea kupata malipo yao kwa njia ya simu ama benki.

Akizungumza Aprili 29, 2025 na mwandishi wa habari hizi ambapo zoezi la malipo linafanyika kwa siku mbili, Mratibu wa TASAF Halmashauri ya Mji Korogwe, Rehema Letara, amesema idadi ya wanaopokea kwa njia ya fedha taslimu inazidi kupungua.

Letara alisema malengo ya TASAF ni kuona walengwa wote wanalipwa kwa njia ya simu au benki, hiyo itarahisisha malipo hayo, lakini pia ni salama na rahisi, tofauti na kutumia fedha taslimu, na wamekuwa wanatumia Benki ya NMB na CRDB kukamilisha zoezi hilo.

"Tunataka walengwa wote waweze kuwa na simu kwa ajili ya malipo. Lakini hata kama mtu ana akaunti ya benki hiyo itakuwa nzuri zaidi. Katika kufanikisha hilo, tunazunguka na maofisa wa Benki ya NMB na CRDB ili kuwaandikisha walengwa waweze kufungua akaunti.

"Na kwa kiasi kikubwa tumefanikiwa, kwani dirisha la malipo ya Januari na Februari, 2025, malipo  ya fedha taslimu ni sh. 8,102,000  kwenye
kaya 261, na malipo ya mtandao (simu) ni kaya 804 ambazo zimelipwa sh. 25,138,000, hivyo kufanya jumla ya  kaya za walengwa wote kuwa 1,065, na jumla ya fedha zote zilizolipwa kwa walengwa kuwa jumla sh. 33,240,000" amesema Letara.

Letara alisema kila kunapofanyika malipo kunakuwa na changamoto zake, lakini yeye pamoja na Afisa Ufuatiliaji wa TASAF (TMO) kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe, na Halmashauri ya Mji Korogwe Elizabeth Mwantyala, wamekuwa wakiwasikiliza walengwa, na kuweza kutatua changamoto hizo.

"Kuna baadhi ya changamoto zinajitokeza kwa walengwa. Wengine huwa wanahama mitaa na kwenda mtaa mwingine. Lakini baadhi yao majina yaliyopo kwenye Kitambulisho cha NIDA hayaendani na majina yaliyopo kwenye kitambulisho cha malipo ya TASAF. 

"Lakini siku hadi siku tumekuwa tunatoa elimu kuwa majina yaliyopo kwenye kitambulisho cha NIDA, ndiyo hayo yawepo kitambulisho cha TASAF na akaunti ya benki ili popote mtu akitafutwa majina yake yote yanasomana" amesema Letara.


Comments

Popular posts from this blog

KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE TAMISEMI YAKOSHWA NA UBORA WA MIRADI YA MAENDELEO KIBAHA TC

MAMBO 10 MAZITO YANAYOIANGAMIZA NA KUIZAMISHA CHADEMA 2024/2025