TARURA BORESHENI BARABARA ZA KATA MAFINGA
Na Mwandishi wetu, DmNewsonline
IRINGA
Baraza la Madiwani la halmashauri ya mji Mafinga limeiomba wakala wa barabara wa mijini na vijijini (TARURA) Wilaya ya MufindI kuboresha Barabara katika kata za halmashauri hiyo ambazo nyingi ziliathiriwa na mvua nyingi iliyonyesha maeneo mbalimbali nchini.
Maswali ya madiwani hayo yameulizwa wakati wakijadili taarifa za kamati za robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2025/2026, wakisema changamoto ya Barabara za kata imekuwa ni kubwa katika halmashauri hiyo hali inayokwamisha wananchi kufanya shughuli za maendeleo.
Akijibu hoja za madiwani hao meneja wa TARURA Wilaya ya Mufindi Muhandisi Nelson Maganga amesema kuwa serikali imejipanga kupeleka tabasamu kwa wananchi kwa kuboresha barabara ambazo hazipitiki huku akiwashauri madiwani kuridhia kuanza kuboresha kwa barabara ambazo zitakuwa na tija kwa watu wengi.
Mwenyekiti wa halmashauri ya mji Mafinga Reginant Kivinge amewapongeza madiwani kwa kuendelea kufuatilia na kuwasilisha changamoto za wananchi kwa weledi mkubwa akisema ofisi yake na mkurugenzi zipo tayari kupokea kero muda wote.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Wilaya ya Mufindi, Robert Kileo akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Linda Salekwa amesema kuwa uhitaji wabarabara kwa wananchi ni mkubwa hivyo ofisi ya mkuu wa wilaya itafuatilia kwa ukaribu kwani changamoto hiyo hata yeye inamkumba katika kata anayoishi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji Mafinga, Bi Fidelica Myovela amesema mapato ya ndani yanayokusanywa yakiunganishwa na fedha za serikali zinazopelekwa husaidia kutekelezwa kwa miradi mbalimbali katika halmashauri hiyo.

Comments
Post a Comment