Kuelekea Siku ya Wauguzi Duniani mamia wazidi kujitokeza Garden kupima afya bure

  Na Eliasa Ally,DmNewsonline

                    IRINGA

KATIKA  hali iliyojawa hamasa, mshikamano na upendo kwa jamii, viwanja vya Garden Manispaa ya Iringa vimegeuka kuwa kitovu cha matumaini baada ya kuanza rasmi kwa shughuli za utoaji bure wa huduma za afya kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wauguzi Duniani, Mei 12 mwaka huu. 

Mamia ya wananchi wamejitokeza kupata huduma mbalimbali huku wakionesha furaha na matumaini mapya juu ya sekta ya afya.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Iringa, Dk. Alfred Mwakalebela, amesema lengo la kupeleka huduma hizo katikati ya mji ni kuwafikia wananchi wengi zaidi na kuondoa hofu iliyojengeka kwa baadhi ya watu kuhusu huduma za afya hospitalini.

Dk. Mwakalebela amesema ni muhimu kwa jamii kuona kuwa wahudumu wa afya ni sehemu yao, watu wanaowajali na wanaotamani kuwaona wakiwa salama kiafya muda wote. 

Amesema huduma hizo si tu tiba, bali ni daraja la kujenga upya imani kati ya wananchi na watumishi wa sekta ya afya.

“Tumefanya shughuli hizi katika maeneo haya ili kuvutia watu wengi zaidi kuja kupata vipimo na kuona kuwa sisi ni sehemu ya jamii yao," amesema na kuongeza;

"Tunataka wananchi wajisikie huru kufika na kupata huduma bila hofu yoyote,” amesema Dkt. Mwakalebela huku akipongezwa na wananchi waliohudhuria uzinduzi huo.

Amewataka wauguzi na watumishi wote wa afya kuhakikisha wanatoa huduma kwa upendo, utu na bila ubaguzi wa aina yoyote. 

Amesisitiza kuwa lugha nzuri na huduma bora kwa wateja ni silaha muhimu ya kurejesha imani kwa wananchi.

Amesema baadhi ya wananchi bado wanaamini kuwa baadhi ya wahudumu wa afya wana lugha kali au isiyofaa, hali inayoweza kuwakatisha tamaa watu kufika hospitalini. 

Kutokana na hilo, amesisitiza umuhimu wa kubadili mtazamo huo kwa kutoa huduma zenye staha, heshima na tabasamu.

Kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu isemayo, “Muuguzi wetu, mustakabali wetu, nguvu ya kiuchumi ya huduma za afya,” imeonekana kuishi kwa vitendo katika viwanja hivyo, ambapo wauguzi na wataalamu mbalimbali wa afya wamekuwa wakitoa huduma kwa kujituma huku wakizungumza kwa karibu na wananchi.

Katika Idara ya Afya ya Mama na Mtoto, wananchi wameendelea kunufaika na huduma za upimaji bure pamoja na uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi, huduma za uzazi wa mpango, ushauri wa afya kwa mama na mtoto pamoja na elimu maalum kwa vijana kuhusu changamoto za ukatili wa kijinsia.

Aidha, Idara ya Magonjwa ya Ndani imeendelea kuwahudumia wananchi kupitia vipimo vya magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo sukari, presha na uzito, huku wataalamu wa afya ya akili wakitoa elimu muhimu ya namna ya kukabiliana na msongo wa mawazo na changamoto nyingine za kisaikolojia. Huduma za lishe pamoja na elimu na upimaji wa virusi vya UKIMWI nazo zimeendelea kutolewa bila malipo.

Kwa upande wa Idara ya Upasuaji, wananchi wamepata nafasi ya kufanyiwa uchunguzi wa macho, meno, kinywa, pua na masikio, huku wengine wakipata ushauri kuhusu matumizi ya viungo bandia na huduma za uchunguzi kwa watoto wachanga, jambo lililowapa wengi fursa ya kugundua changamoto za afya mapema.

Wananchi waliojitokeza wamepongeza hatua hiyo wakisema imeleta matumaini mapya kwa watu ambao kwa muda mrefu walikuwa wakisita kwenda hospitali kutokana na gharama au hofu ya namna watakavyopokelewa. Wengi wameeleza kuwa huduma hizo zimeonyesha sura mpya ya sekta ya afya yenye ukaribu na jamii.

Maadhimisho hayo yameendelea kuwa zaidi ya sherehe; yamekuwa darasa la utu, upendo na uwajibikaji kwa jamii. 

Kupitia juhudi hizo, Iringa imeonyesha kuwa muuguzi si tu mtoa huduma wa afya, bali ni nguzo ya matumaini, mshauri wa maisha na sehemu muhimu ya maendeleo ya taifa.   

Comments

Popular posts from this blog

UONGOZI WA SHIRIKISHO LA VYAMA VYA TIBA ASILI TANZANIA WADAIWA SI HALALI NA UMEKOSA DIRA YA KUENDESHA VYAMA VYA WAGANGA WA TIBA ASILI

DKT. KIJAZI KUSIMAMIA MIRADI YA MAENDELEO JIMBO LA KOROGWE MJINI.