KIBAHA MANISPAA KUCHUKUA HATUA YA KUKABILI CHANGAMOTO YA MAJI.

Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha Dkt .Mawazo Nicas akizungumza katika kikao cha Baraza la Madiwani lililofanyika Mei 12/2026 katika jengo la Halmashauri hiyo na kushoto ni Mkurugenzi wa Manispaa Dkt.Rogers Shemwelekwa na wa kwanza Kulia ni Naibu Meya wa Manispaa Aziza Mruma.

NaGustaphu Haule,DmNewsonline

                     PWANI 

BARAZA la Madiwani la Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha limepanga kuchukua hatua ya dharula ya kutatua  changamoto ya maji kwa kuchimba visima vya maji na kupeleka matenki ya maji katika Kata ambazo zimekuwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa hudumal ya maji.

Mbali na kutatua changamoto ya maji lakini pia baraza hilo limepanga kutatua changamoto ya barabara zake za ndani kwa  kuhakikisha wanaanza kujenga barabara hizo kwa kiwango cha lami japo kidogo kidogo.

Mipango ya utatuzi wa changamoto hizo imefanyika katika kikao cha kikanuni cha Baraza la Madiwani lililofanyika Mei 12/2026 lililolenga kupokea taarifa za kamati za utekelezaji wa shughuli mbalimbali katika kipindi cha robo ya tatu ya Mwaka 2025/2026.

Hatua hiyo imekuja mara baada ya kubaini kuwa katika Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha baadhi ya Kata ikiwemo Kata ya Viziwaziwa,Kata ya Pangani na Kata ya Msangani ndizo Kata ambazo zenye changamoto kubwa ya upatikanaji wa maji.

Meya wa Manispaa ya Kibaha Dkt.Mawazo Nicas amesema kuwa changamoto ya maji ni kubwa katika baadhi ya maeneo na kwamba ili kukabiliana na hali hiyo ni lazima waanze kuchukua hatua ya dharula ya kuchimba visima vya maji ili kuwasaidia Wananchi.

Dkt.Nicas amesema kuwa Baraza limebaini moja ya changamoto ya Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha ni ukosefu wa maji katika Kata tofauti tofauti na sasa tayari wamekubaliana na Dawasa kupelekea matenki ya maji katika maeneo yenye ukosefu wa maji kwa udharula ili kuwasaidia Wananchi.

Amesema Wananchi watakuwa wanalipia maji hayo kwa bei nafuu ya Sh.50 hadi 100 huku akisema pamoja na kupeleka matenki ya maji katika maeneo hayo ,lakini pia wamekubaliana kuchimba visima  vya maji ili kurahisisha upatikanaji zaidi wa huduma ya maji kwa Wananchi.

Amesema wakati matenki yamepelekwa na visima vimechimbwa bado kutakuwa na mipango ya muda mrefu ya utekelezaji wa miradi mikubwa ya maji ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kama ambavyo Waziri wa Maji Jumaa Aweso alivyosema lengo ni kumtua mama ndoo kichwani.

Kuhusu barabara Meya huyo amesema kuwa  Manispaa ya Kibaha hadi sasa ina Kilomita 21 za lami kati ya Kilomita zaidi ya 500 zilizopo na kwamba barabara nyingi zimekuwa za udongo ambazo kila mwaka zinakarabatiwa na kuchongwa lakini inapofika mvua huwa zinaharibika tena.

Amesema jambo hilo linasababisha fedha nyingi kupotea bila sababu ambapo kutokana na hali hiyo baraza litakuja na mpango wa kutengeneza barabara hizo kwa kiwango cha lami japo kidogo kidogo ili kuepusha mambo ya kila mwaka kutenga fedha kwa ajili ya kuchonga barabara hizo.

Dkt.Nicas amesema ujenzi wa barabara hizo watatumia zaidi wakandarasi wa ndani ambao watakuwa wanalipwa kidogo kidogo kutokana na fedha za mapato ya ndani na lengo hasa ni kutengeneza uso wa Manispaa ya Kibaha.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha Dkt.Rogers Shemwelekwa amesema yale yote yaliyojadiliwa na madiwani ameyachukua na atakwenda kukaa na timu yake kwa ajili ya kuweka mipango ya namna ya kuanza utekelezaji wake.

Dkt.Shemwelekwa amesema kuwa anamshukuru Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha Dkt.Mawazo Nicas kwa kuendesha vikao vizuri na kwamba amefarijika  kuona kila diwani aliyesimama amechangia mambo muhimu (issues) ya kuijenga Manispaa kimaendeleo.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kibaha Mjini Mwajuma Nyamka, amepongeza Meya wa Manispaa ya Kibaha Dkt.Mawazo Nicas kwa namna ambavyo ameendesha vikao vya Baraza hilo huku akisema inatia moyo ya kuona Manispaa inakwenda kuwa namba moja nchini.

 Nyamka amefafanua ili Manispaa iweze kwenda vizuri zaidi ni vyema madiwani na watumishi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha wakaendeleza Upendo,Umoja na Mshikamano kama ambavyo Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan anavyosisitiza
Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha Dkt.Rogers Shemwelekwa akizungumza katika kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika Mei 12/2026
Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha wakiwa katika kikao chao kilichofanyika Mei 12/2026 kwa ajili ya kujadili shughuli za utekelezaji wa maendeleo katika kipindi cha Robo ya tatu ya mwaka 2025/2026
Diwani wa viti maalum Selina Msenga wa kwanza kulia akiteta jambo na diwani wa viti maalum Sarah Uled katika kikao cha baraza la madiwani la Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha kilichofanyika Mei 12/2026 ,Selina ni Mhariri Makala wa kampuni ya Uhuru Media

Comments

Popular posts from this blog

UONGOZI WA SHIRIKISHO LA VYAMA VYA TIBA ASILI TANZANIA WADAIWA SI HALALI NA UMEKOSA DIRA YA KUENDESHA VYAMA VYA WAGANGA WA TIBA ASILI

DKT. KIJAZI KUSIMAMIA MIRADI YA MAENDELEO JIMBO LA KOROGWE MJINI.