TANGA MWENYEJI WA MAADHISHO YA KITAIFA SIKU YA HAKI ZA MTUMIAJI 2026.
Na Angelina Mganga ,DmNewsOnline
Dar es Salaam
MWENYEKITI wa Jukwaa la Watumiaji Tanzania (TCF), D.G. Daudi, amesema kuwa usalama wa bidhaa na huduma ni haki ya msingi kwa watumiaji wote. Amesisitiza kuwa watumiaji wenye kujiamini ni wale wanaojua haki na wajibu wao, na hivyo wanadhibitiwa na wanazozihitaji.
Katika kuadhimisha siku hii, Jukwaa la Watumiaji Tanzania (TCF) litaendesha shughuli mbalimbali za utoaji elimu kwa umma kuanzia tarehe 10 hadi 15 Machi 2026. Shughuli hizi zimeundwa kuelimisha watumiaji kuhusu haki zao na jinsi ya kutumia huduma zinazodhibitiwa.
Amesema maadhimisho ya mwaka huu yataweka msisitizo katika masuala ya usalama wa huduma na bidhaa, ikiwa ni pamoja na huduma salama za nishati na maji zinazohusisha viwango vya ubora na kulinda maslahi ya watumiaji pamoja na mazingira.
Aidha ameeleza kuwa shughuli zitajumuisha elimu kuhusu usalama wa watumiaji wa anga na vifaa vya usalama na usalama wa watumiaji wa nchi kavu unaozingatia viwango vya usalama na haki za watumiaji.
Jukwaa la Watumiaji Tanzania (TCF) limewahimiza wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za maadhimisho haya ili kupata elimu kuhusu haki na wajibu wao katika kutumia huduma zinazodhibitiwa na maslahi ya kuhifadhi haki zao kama watumiaji.
Hata hivyo amewakaribisha Wananchi wa Jiji la Tanga na maeneo ya jirani kushiriki katika maadhimisho hayo yatakayofanyika katika Ukumbi wa Mkurugenzi wa Jiji, ambapo pamoja na hafla ya kilele kutakuwa na maonesho na utoaji wa elimu kwa umma kuhusu haki na wajibu wa watumiaji wa huduma zinazodhibitiwa.
Kupitia maonesho hayo, wananchi watapata fursa ya kujifunza zaidi kuhusu huduma mbalimbali zinazodhibitiwa, taratibu za kuwasilisha malalamiko pamoja na namna ya kulinda haki zao kama watumiaji.

Comments
Post a Comment