SERIKALI YAWATAKA WATUNZA NYARAKA KUFANYA KAZI KWA WELEDI NA UADILIFU
Na Timothy Marko, DmNewsonline
DAR ES SALAAM
SERIKALI imewataka watumishi wa umma wanaoshughulika na utunzaji wa nyaraka kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa weledi, uadilifu na kuzingatia matumizi ya mifumo ya kisasa ya kidijitali ili kulinda taarifa nyeti za taifa.
Wito huo umetolewa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, wakati wa kufungua Mkutano wa 13 wa Chama cha Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka (TRAMPA) uliofanyika jijini Dar es Salaam. Amesema utunzaji wa nyaraka za Serikali ni uti wa mgongo wa maendeleo ya taifa, hasa kuelekea Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050.
“Watunza nyaraka ni wasimamizi muhimu wa dira ya maendeleo ya taifa letu. Serikali ya Awamu ya Sita inalenga kuhakikisha nyaraka zote za serikali zinatunzwa kwa usahihi, usalama, usiri na kwa kutumia mifumo ya kidijitali,” amesema Waziri Mkuu Majaliwa.
Aidha, amesisitiza kuwa mifumo ya utunzaji nyaraka isomeane kwa njia ya mtandao (interoperability) ili kuongeza ufanisi wa mawasiliano na usimamizi wa kumbukumbu serikalini.
Katika hatua nyingine, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene, alieleza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana kwa karibu na TRAMPA katika kuimarisha taaluma ya usimamizi wa nyaraka. Alisema mkutano huo ni jukwaa muhimu kwa wataalamu kubadilishana uzoefu na kukuza ufanisi wa kiutumishi.
“Tunatambua nafasi ya watunza kumbukumbu katika kulinda historia na taarifa za Serikali. Ofisi ya Rais itaendelea kushirikiana na TRAMPA kuhakikisha kazi hii inafanywa kwa weledi, uwazi na maadili ya hali ya juu,” amesema Simbachawene.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TRAMPA, Bi. Devota Mrope, alisema chama hicho kina jumla ya wanachama 8,000, ambapo takribani 3,000 walihudhuria mkutano huo. Alibainisha kuwa TRAMPA itaendelea kuandaa mafunzo na mikutano ya kitaaluma kila mwaka kwa lengo la kuwajengea uwezo wataalamu wa nyaraka kote nchini.
“Watunza kumbukumbu ndio wabeba maono ya taifa. Bila taarifa, hakuna sera, mipango wala maendeleo ya kweli. Ndio maana tunasisitiza utunzaji wa taarifa kwa uaminifu na kwa kutumia teknolojia za kisasa,” amesema Mrope.
Kaulimbiu ya mkutano huo ilikuwa: “Matumizi ya Ofisi Mtandao katika Kuimarisha Ushiriki wa Uchaguzi Mkuu”, ikiakisi umuhimu wa mifumo ya TEHAMA katika kuhakikisha usalama na upatikanaji wa taarifa kwa wakati.
Mkutano huo umefanyika wakati Serikali ikiendelea kuwekeza kwenye mifumo ya kidijitali na kutoa mafunzo kwa watendaji serikalini, ili kuhakikisha taarifa za Serikali zinalindwa na zinapatikana kwa urahisi wakati wowote. 

Comments
Post a Comment