SEKTA YA KILIMO YAINUA MAISHA YA WAKAZI KASULU


  Na Allan Kitwe,DmNewsonline

              KASULU

HALMASHAURI ya Mji Kasulu ni miongoni mwa halmashauri 8 za Mkoa wa Kigoma ambapo asilimia 80 ya wakazi wake wanaishi Vijijini na shughuli kuu ya kiuchumi katika maeneo hayo ni kilimo.

Maboresho makubwa ya sekta ya kilimo yaliyofanywa na serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dk Samia Suluhu Hassan yameleta tija kubwa kwa wakazi wa halmashauri hiyo na Wilaya nzima ya Kasulu.

Akiongea na gazeti hili hivi karibuni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Vumilia Simbeye ameeleza kuwa katika kipindi cha miaka 4 ya uongozi wa Rais Samia, halmashauri hiyo imepiga hatua kubwa kimaendeleo kupitia sekta hiyo.

Amebainisha mambo yaliyofanywa na serikali ya awamu ya sita ambayo yamechochea mafanikio makubwa kwa wakazi wa halmashauri hiyo kuwa ni kuongezwa bajeti, ugawaji mbolea ya ruzuku na kutafuta masoko ya kutosha.

Haya yamepelekea wakazi wengi wa halmashauri hiyo kuchangamkia sekta ya kilimo hali ambayo imepelekea uzalishaji mazao ya chakula na biashara kuongezeka mara dufu hivyo kuongeza mapato ya wakulima na halmashauri.

Simbeye ametaja mazao ya chakula ambayo yanalimwa kwa wingi sana na wakazi wa halmashauri hiyo na kuwaingizia kipato kikubwa kuwa ni maharage, mahindi, mbaazi, udaga/kambaranga, mhogo mbichi, karanga na mpunga.

Kutokana na maboresho hayo kwa mwaka wa fedha 2023/2024 sekta hiyo iliwezesha halmashauri kuingiza zaidi ya sh milioni 379.3 baada ya kuzalishwa magunia 189,684 sawa na tani 18,968 (kilo 18,968, 475) ambapo wakulima walivuna zaidi ya sh bilioni 33.1.

Amedokeza kuwa kwa mwaka wa fedha 2024/2025 mapato ya halmashauri yaliongezeka hadi kufikia sh milioni 446.9 baada ya kuzalishwa magunia 223,493 sawa na tani 22,350 (kilo 22,349,350) ambapo wakulima walivuna sh bilioni 35.5.

Mkuu wa Idara ya Kilimo na Mifugo katika Halmashauri hiyo Dk Sabinus Chaula ameeleza kuwa pembejeo za ruzuku zilizotolewa na serikali ya awamu ya sita kwa wananchi zimeleta mageuzi makubwa katika sekta hiyo kwa kuongeza uzalishaji.

Amebainisha mazao ya kimkakati ambayo yamepewa kipaumbele kikubwa na kuanza kulimwa na wakazi wa halmashauri hiyo kwa ajili ya biashara kuwa ni kahawa na michikichi.   


Comments

Popular posts from this blog

KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE TAMISEMI YAKOSHWA NA UBORA WA MIRADI YA MAENDELEO KIBAHA TC

NAIBU WAZIRI NDERIANANGA AONGOZA UJUMBE WA TANZANIA KATIKA MKUTANO WA TATU WA KIMATAIFA WA WATU WENYE ULEMAVU UJERUMANI.