MAONESHO YA KILIMO KANDA YA MAGHARIBI KUFANYIKA TABORA AGOSTI 1-8
Na Allan Kitwe, DmNewsonline
TABORA
TAASISI mbalimbali, wadau wa maendeleo na wakazi wa Mikoa ya Tabora, Kigoma na Mikoa jirani wametakiwa kujitokeza kwa wingi katika maonesho ya wakulima nane nane Kanda ya Magharibi ambayo yanatarajiwa kuanza Agosti 1-8.
Hayo yamebainishwa leo na Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora Dk. John Mboya alipokuwa akiongea na vyombo vya habari Ofisini kwake ambapo alibainisha kuwa maonesho ya mwaka huu yamesheheni mambo mengi mazuri.
Amesema kuwa maonesho hayo ya sikukuu ya wakulima hufanyika kila mwaka hapa nchini na kwa Kanda ya Magharibi yanafanyika katika Viwanja vya Nane Nane Ipuli Mjini Tabora na kushirikisha Mikoa miwili ya Tabora na Katavi.
Dkt. Mboya amefafanua kuwa maonesho hayo yenye kauli mbiu isemayo ‘Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi: Viongozi Bora ndiyo msingi wa maendeleo.
Ametaja taasisi zilizoshiriki maonesho ya mwaka jana kuwa ni za sekta ya umma, binafsi, halmashauri za Mkoa wa Tabora na Kigoma, taasisi za serikali, majeshi, utafiti, makampuni ya simu, taasisi zisizo za serikali na tasisi za fedha.
‘Natoa wito kwa wakazi wote wa Mikoa ya Tabora na Kigoma na maeneo jirani kujitokeza kwa wingi kushiriki katika maonesho haya ili kunufaika na fursa lukuki zilizopo ikiwemo kujipatia bidhaa bora za wakulima na wajasiriamali, ameeleza.
Dk Mboya amedokeza kuwa waliohudhuria maonesho ya mwaka jana walipata manufaa mengi, ikiwemo elimu, teknolojia za kilimo na ufugaji, fursa za masoko na kuongeza mnyororo wa thamani kwa bidhaa za mazao, mifugo na uvuvi.
Amesisitiza kuwa maonesho hayo ni fursa muhimu sana kwa taasisi, wakulima, wafanyabiashara na wadau mbalimbali kuonesha bidhaa wanazozalisha na kuziuza, kuonesha uwezo wao wa kuendeleza sekta ya kilimo.
Aidha kupitia vipando, wakulima na wadau wote wataweza kujua na kujifunza taknolijia bora za uzalishaji bidhaa zilizopo hapa nchini, wakulima na wadau wengine watapata taarifa kuhusu sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi.
RAS ameongeza kuwa Viongozi wa kitaifa watakaoshiriki maonesho hayo kama wageni rasmi watapata wasaa wa kutoa maagizo na maelekezo yenye tija kwa wananchi. 





Comments
Post a Comment