ESTER JEMSI AWAOMBA KURA WANACHIKOBE NA NYACHILULUMA, AAHIDI KUJA NA MFUKO MAALUMU WA KUSAIDIA WANAFUNZI WAISHIO MAZINGIRA MAGUMU
Na Mwandishi wetu, DmNewsonline
GEITA
MGOMBEA wa ubunge Jimbo la Katoro kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ester Jemsi, amewaomba wanachama wa chama hicho katika kata za Bukondo na Nyachiluluma kumpa ridhaa ya kuwa mbunge wao, akiahidi kuwa ataleta maendeleo yenye tija kwa wananchi wa jimbo hilo.
Akizungumza mbele ya wajumbe wa CCM kwenye kata hizo, Ester amesema ana ndoto kubwa ya kulifanya Jimbo la Katoro kuwa eneo la kuvutia kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi, endapo atapewa nafasi ya kuliongoza.
"Naomba niaminiwe. Nina ndoto ya kuona Katoro inabadilika, na nina nia ya dhati kuhakikisha wananchi wananufaika na rasilimali zao," amesema Ester.
Ester Jemsi amebainisha kuwa moja ya mipango yake ni kuanzisha mfuko maalumu wa kusaidia wanafunzi wanaoishi katika mazingira magumu, akisema tayari alikuwa akitekeleza mpango huo akiwa kiongozi wa vijana, lakini sasa analenga kuupanua ufikie jimbo zima.
"Tuna watoto wengi ndani ya jimbo letu wanaosoma katika mazingira magumu. Naahidi kuwa kila mwezi wa Juni na Desemba, nitatoa msaada wa vifaa vya shule kupitia mfuko huo," amesema.
Mbali na hilo, Ester ameahidi kusimamia utekelezaji wa ilani ya CCM kwa ukamilifu, kwa kushirikiana na wananchi na viongozi wa serikali katika kila hatua ya maendeleo.
"Ilani ya CCM imejieleza vizuri. Kila eneo linaeleza nini tunatakiwa kufanya,Nitahakikisha yote yanatekelezwa ipasavyo kwa faida ya wananchi wetu," amesisitiza.






Comments
Post a Comment