ULYANKULU WAPONGEZA KASI YA RAIS SAMIA KUBORESHA ELIMU
Na Allan Kitwe,DmNewsonline
KALIUA
WAKAZI wa Tarafa ya Ulyankulu, Jimbo la Ulyankulu, Wilayani Kaliua Mkoani Tabora wamepongeza juhudi kubwa zinazoendelea kufanywa na serikali ya awamu ya 6 kwa kuboresha miundombinu ya elimu katika vijiji na kata zote.
Wakizungumza na mwandishi wa gazeti hili kwa nyakati tofauti wameeleza kuwa Tarafa hiyo ni miongoni mwa tarafa zilizokuwa na shule chache na miundombinu hafifu lakini kasi ya serikali ya awamu ya 6 imeleta neema kubwa Jimboni humo.
Mkazi wa Kata ya Ichemba Annaemmy Mazigo ambaye pia ni Mkuu wa shule ya sekondari Mkindo amempongeza Rais wa awamu ya 6 Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuipa sekta ya elimu kipaumbele kikubwa na kutenga bajeti ya kutosha.
Ameeleza kuwa katika shule ya Mkindo sekondari amepeleka zaidi ya sh mil 500 kwa ajili ya ujenzi wa mabweni 4 na matundu 10 ya vyoo ili kuboresha miundombinu ya shule hiyo na kuwezesha watoto wengi kukaa shuleni.
‘Kujengwa kwa mabweni haya kumeleta ari na hamasa kubwa kwa watoto wa kike na kiume kupenda shule, hata utoro sasa hivi umepungua sana na kila mtoto anasoma kwa bidii ili aweze kutimiza ndoto zake’, ameeleza.
Mkazi wa Tarafa hiyo Ashura Mohamed ambaye ni Mwenyekiti wa UWT Kata ya Mwongozo amedokeza kuwa vijiji na kata nyingi katika Jimbo hilo vilikuwa havina shule za msingi wala sekondari lakini sasa shule zimejengwa katika kata na vijiji.
Amemshukuru Rais Samia kwa kupeleka zaidi ya sh mil 360 katika mwaka wa fedha uliopita ili kujengwa shule mpya ya msingi Langoni katika Kijiji cha Ibambo katika Kata hiyo ili kupunguza mlundikano wa watoto katika shule ya Ibambo.
Mbunge wa Jimbo hilo Rehema Migira amefafanua kuwa wana kila sababu ya kumshukuru Rais Samia kwa kuwapatia mabilioni ya fedha kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya, mabweni, madarasa, matundu ya vyoo na nyumba za walimu.
Amebainisha kuwa katika kipindi cha miaka 4 tu ya utawala wake kata zote 15 za Jimbo hilo zimepata shule za sekondari na shule za msingi zimeendelea kujengwa katika vijiji vyote ikiwemo kuboreshwa miundombinu ya shule zote.
Mkuu wa Wilaya hiyo Dkt Gerald Mongela naye ameeleza wazi kuwa wakazi wa Tarafa hiyo na Wilaya nzima ya Kaliua wanajivunia mambo makubwa yaliyofanywa na Rais Samia kwa kuboresha huduma za kijamii katika sekta zote.
Amesisitiza kuwa shukrani za wana Kaliua zimeonekana kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka jana ambapo CCM ilipata ushindi wa asilimia 99 na kuahidi kuwa uchaguzi mkuu wa mwaka huu Rais Samia atapata kura za kishindo.
Comments
Post a Comment